Hizbullah: Saudia imekiri yenyewe kwamba imeshindwa nchini Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i34205-hizbullah_saudia_imekiri_yenyewe_kwamba_imeshindwa_nchini_syria
Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sheikh Naim Qassim amesema kuwa, hatua ya Wizara ya Mambo ya Nje ya SaudiArabia ya kukubali kuanzishwa maeneo ya kupunguza mivutano nchini Syria, ina maana ya kukiri wazi Riyadh juu ya kushindwa kwake nchini Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 11, 2017 03:52 UTC
  • Hizbullah: Saudia imekiri yenyewe kwamba imeshindwa nchini Syria

Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sheikh Naim Qassim amesema kuwa, hatua ya Wizara ya Mambo ya Nje ya SaudiArabia ya kukubali kuanzishwa maeneo ya kupunguza mivutano nchini Syria, ina maana ya kukiri wazi Riyadh juu ya kushindwa kwake nchini Syria.

Jumapili ya jana Adel al-Jubeir, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia na katika kikao na waandishi wa habari mjini Jeddah pamoja na waziri mwenzake wa Russia, Sargey Lavrov, ikiwa ni miaka sita ya vita nchini Syria na baada ya kushindwa makundi ya kigaidi kwa ajili ya kuiondoa madarakani serikali ya Damascus, alisema kuwa Saudia inakubaliana na pendekezo la kuanzishwa maeneo ya kupunguza mizozo nchini humo.

Adel al-Jubeir alipokutana na Sargey Lavrov mjini Jeddah Saudia

Hadi sasa kumefanyika duru tano za mazungumzo mjini Astana, mji mkuu wa Kazakhstan kwa kuhudhuriwa na timu za wawakilishi wa serikali na wapinzani wa Syria ambapo pande mbili zilikubaliana kusitisha mapigano chini ya usimamizi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Uturuki na Russia. Lengo kuu la mazungumzo hayo ni kutiwa saini makubaliano yenye lengo la kuanzishwa maeneo ya kupunguza migogoro nchini Syria. Kufuatia hali hiyo Sheikh Naim Qassim akizungumza na kanali ya televisheni ya al-Manar amesema kuwa, Saudia inapitia wakati na kipindi kigumu kutokana na kushindwa mipango yake yote katika eneo la Mashariki ya Kati. Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameashiria kuwa, muqawama nchini Syria umekuwa ukisajili ushindi na kwamba ushindi huo utaendelea

Jeshi la Syria likizidi kupata mafanikio zaidi dhidi ya magaidi vibaraka

Ameongeza kuwa, kukombolewa mji wa Aleppo kumefelisha njama za maadui za kutaka kuigawa vipande nchi ya Syria na kwamba kukombolewa mji wa Deir ez-Zor, ni ushindi mwingine mkubwa dhidi ya genge la kigaidi la Daesh. Mji wa Aleppo ambao kwa miaka kadhaa ulikuwa ukidhibitiwa na magaidi wanaoungwa mkono na Marekani, Israel, Saudia na kadhalika ulikombolewa mwezi Disemba mwaka jana baada ya mapigano makali na jeshi la Syria likishirikiana na harakati ya Hizbullah dhidi ya magaidi wa Dadesh.