UN yataka ufanyike uchunguzi kuhusu ukiukaji haki za binadamu uliofanywa Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i34251-un_yataka_ufanyike_uchunguzi_kuhusu_ukiukaji_haki_za_binadamu_uliofanywa_yemen
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametaka ufanyike uchunguzi wa kimataifa kuhusu ukiukaji haki za binadamu uliofanywa katika vita vya Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 12, 2017 03:15 UTC
  • UN yataka ufanyike uchunguzi kuhusu ukiukaji haki za binadamu uliofanywa Yemen

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametaka ufanyike uchunguzi wa kimataifa kuhusu ukiukaji haki za binadamu uliofanywa katika vita vya Yemen.

Zeid Ra’ad al-Hussein amesema, kutokana na Umoja wa Mataifa kuthibitisha kuwa raia 5,144 wameuliwa katika uvamizi wa kijeshi uliofanywa dhidi ya Yemen, ambapo akthari yao wamepoteza maisha kutokana na mashambulio ya anga ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kuna umuhimu mkubwa wa suala hilo kufanyiwa uchunguzi wa kimataifa.

Akihutubia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva hapo jana, Zeid amesema uharibifu uliofanywa nchini Yemen na masaibu yaliyowapata watu wa nchi hiyo yatakuwa na taathira kubwa kwa eneo zima la Mashariki ya Kati na kusisitiza kwamba juhudi zilizofanywa kukabiliana na hatari ya ukiukaji wa kila leo wa haki za binadamu katika vita vya Yemen hazitoshi.

Maafa ya roho za watu yanashuhudiwa kila leo Yemen kutokana na mashambulio ya Saudia

Hii ni mara ya pili kwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa kutaka ufanyike uchunguzi wa kimataifa kuhusiana na ukiukaji haki za binadamu uliofanywa nchini Yemen.

Mashambulio ya anga ya usiku na mchana ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen, yaliyoanzishwa mwezi Machi mwaka 2015 na kuendelea hadi sasa yameshaua watu zaidi ya 12,000, na kuwafanya wengine zaidi ya milioni tatu wabaki bila ya makaazi. Madhumuni ya  vita hivyo vinavyoendelea kwa uungaji mkono wa Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu ni kuisambaratisha harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah na kumrejesha madarakani Abd Rabbuh Mansur Hadi, kibaraka wa Aal Saud ambaye  alikuwa rais lakini akajiuzulu na kuitoroka nchi.../