Sudan yaitupa mkono Saudia, sasa yakusudia kuimarisha zaidi mahusiano na Qatar
(last modified Sat, 16 Sep 2017 03:32:39 GMT )
Sep 16, 2017 03:32 UTC
  • Sudan yaitupa mkono Saudia, sasa yakusudia kuimarisha zaidi mahusiano na Qatar

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ameeleza kuwepo mazungumzo kati ya Sudan na Qatar kwa ajili ya kupanua zaidi mahusiano ya pande mbili.

Qaribullah Khidhr amesema kuwa tayari Abdul-Ghani al-Naim, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan amekutana na Rashid Abdulr-Rahman al-Naimi, balozi wa Qatar mjini Khartoum na kuzungumzia suala la kuinua kiwango cha mahusiano ya nchi mbili. Akiashiria mahusiano mazuri kati ya Doha na Khartoum, Khidhr amesema kuwa mwezi Oktoba ujao Sudan na Qatar zitafanya kikao mjini Doha kwa ajili ya kuboresha mahusiano yao.

Amir wa Qatar

Aidha Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan amesema kuwa, baada ya kuibuka mgogoro kati ya nchi za Kiarabu na Qatar, serikali ya Sudan iliamua kutopendelea upande wowote na badala yake imekuwa ikiunga mkono juhudi za upatanishi za Kuwait kuhusiana na suala hilo. Baada ya kuibuka mgogoro kati ya nchi za Kiarabu, Saudia ilizishawishi nchi mbalimbali kufuata sera za Riyadh katika kuisusia Qatar ambapo nchi kadhaa zilikubaliana na pendekezo hilo.

Mfalme wa Saudia

Mbali na Sudan kukataa kuwa upande wa Saudia, hivi karibuni pia Rais wa Somalia alitangaza kukataa pendekezo la kupewa kiasi cha Euro milioni 68 lililotolewa na utawala wa Kifalme wa Saudi Arabia mkabala wa kujiunga na muungano wa nchi zilizokata uhusiano wao na Qatar. Saudia pamoja na nchi nyingine tatu za Kiarabu zilikata uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar kwa tuhuma kwamba nchi hiyo inaunga mkono ugaidi na haifuati sera za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi linaloongozwa na Riyadh katika mahusiano yake ya kigeni.

Tags