Njama mpya za Saudi Arabia dhidi ya Qatar
Mwanamfalme, Abdullah bin Ali Aal Thani kutoka familia ya kifalme ya Qatar amekosoa siasa za Amir wa nchi hiyo, Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani na kumtaka aitishie kikao cha kitaifa cha kujadili mgogoro wa nchi hiyo.
Mwanamfalme huyo wa Qatar amewaambia wananchi wa nchi hiyo kwamba: Ninasikitika sana kuona hali ya Qatar inazidi kuwa mbaya. Hayo ni matokeo ya nchi yetu kufanya uchochozi dhidi ya utulivu wa nchi za Kiarabu na kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine. Nchi zote zinazofanya chokochoko kama hizo hazina mwisho mwingine isipokuwa kutumbukia katika mizozo na migogoro.
Matamshi hayo ya Abdullah bin Ali Aal Thani dhidi ya watawala wa hivi sasa wa Doha yametolewa na mtu ambaye anauangalia kwa jicho la tamaa uongozi wa Qatar na hayakutolewa na raia wa kawaida wa nchi hiyo. Tuhuma hizo zinaakisi moja kwa moja tuhuma zinazotolewa na serikali ya Saudia dhidi ya Qatar. Abdullah bin Ali anamshambulia moja kwa moja Amiri wa Qatar na kumsifu Mfalme Salman wa Saudi Arabia. Hivyo inaonekana wazi kwa, Abdullah bin Ali ana hamu ya kukalia kiti cha ufalme wa Qatar kwa gharama yoyote ile. Kwa upande wake, Saudi Arabia imeonesha wazi hamu yake ya kuupindua utawala wa hivi sasa wa Qatar na ndio maana imekuja na opesheni mpya ya kutafuta na kumtia nguvu mtu mwingine wa kuvaa taji la ufalme wa Qatar.
Saudia iliongoza muungano wa nchi nne za Kiarabu za Bahrain, Imarati na Misri kuweka vikwazo vikali sana dhidi ya Qatar ikiwa ni pamoja na kuifungia nchi hiyo njia zote za angani, ardhini na baharini kwa tamaa kwamba Doha ingelisalimu amri masaa machache tu baadaye. Hata hivyo zilichokisahau nchi hizo nne za Kiarabu ni kwamba, Qatar ilikuwa na machaguo mengine ambayo huenda ni bora zaidi. Baada ya Riyadh kushindwa katika njama zake dhidi ya Doha, imeamua kuja na mkakati mpya wa kuipindua serikali ya Doha nao ni kuwachochea baadhi ya watu wa familia ya kifalme ya Qatar kusimama dhidi ya serikali ya nchi hiyo. Kampeni kubwa inayofanywa na Saudi Arabia hivi sasa ni kumuonesha mwana mfalme Abdullah bin Ali Aal Thani kuwa ni mwokozi wa wananchi wa Qatar katika mgogoro mkubwa iliotumbukia nchi hiyo. Hata wakati wa msimu wa Hija, Mfalme Salman wa Saudi Arabia alimtumia Abdullah bin Ali kama mpatanishi wa kuruhusu kufunguliwa mpaka wa ardhini wa Saudia na Qatar kwa ajili ya mahujaji wa nchi hiyo.
Amma swali linalojitokeza hapa ni kwamba, ni kwa nini Saudi Arabia imemchagua Abdullah bin Ali kuwa mfanikishaji wa njama zake mpya dhidi ya Qatar? Sababu kubwa ni kwamba Abdullah bin Ali ni mwana wa Ali bin Abdullah Aal Thani, amiri wa nne wa Qatar. Ukoo wa Abdullah bin Ali ulipinduliwa na babu mzaa baba wa amiri wa hivi sasa wa Qatar mwaka 1972 kupitia mapinduzi ya kijeshi. Hivyo kwa upande mmoja, Abullah bin Ali ni kutoka ukoo uliowahi kutawala Qatar huko nyuma na wakati huo huo ni kutoka watu ambao walipinduliwa kijeshi na watawala walioko madarani leo hii nchini Qatar. Hivyo baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema bila kigugumizi kwamba, lengo kuu la Saudi Arabia ni kufufua majeraha ya huko nyuma, kuchochea ugomvi na kueneza fitna ndani ya ukoo wa kifalme wa Qatar.
Hata hivyo, serikali ya Qatar inaonekana imejiandaa vilivyo kusimama imara kukabiliana na njama hizo za Saudia dhidi yake. Safari ya mfalme wa Qatar iliyofanyika tarehe 14 na 15 mwezi huu ya kuzitembelea nchi za Uturuki, Ujerumani na Ufaransa, ilikuwa ni ujumbe wa wazi kwa Saudi Arabia kwamba si tu serikali ya Doha ina uungaji mkono mkubwa kimataifa, lakini pia ni imara ndani ya Qatar kiasi kwamba mfalme wa nchi hiyo anajiamini kuondoka nchini humo bila ya kuhofia kupinduliwa wakati akiwa nje ya nchi.