Jamii ya kimataifa yapinga kura ya maoni ya kujitenga Kurdistan, Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i34719-jamii_ya_kimataifa_yapinga_kura_ya_maoni_ya_kujitenga_kurdistan_iraq
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Alkhamisi iliyopita lilipasisha azimio lililopinga suala la kuitishwa kura ya maoni kwa ajili ya kujitenga eneo la Kurdistan huko kaskazini mwa Iraq.
(last modified 2025-10-11T08:57:00+00:00 )
Sep 23, 2017 02:34 UTC
  • Jamii ya kimataifa yapinga kura ya maoni ya kujitenga Kurdistan, Iraq

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Alkhamisi iliyopita lilipasisha azimio lililopinga suala la kuitishwa kura ya maoni kwa ajili ya kujitenga eneo la Kurdistan huko kaskazini mwa Iraq.

Eneo la Kurdistan la Iraq linatazamiwa kupiga kura ya maoni ya kujitenga na Iraq tarehe 25 mwezi huu wa Septemba, hatua ambayo imepingwa vikali na serikali kuu ya Iraq, makundi mbalimbali ya kisisa nchini humo na nchi karibu zote za Mashariki ya Kati.

Kwa kutilia maanani upinzani huo wa ndani, wa kikanda na kimataifa dhidi ya kura ya maoni ya kujitenga eneo la Kurdistan, inatazamiwa kuwa wiki ijayo itashuhudia matukio mengi muhimu huko Iraq. Katika uwanja huo kituo cha habari cha al A'hd kimechapisha makala iliyoandikwa na mchambuzi wa Iraq, Adil al Jaburi akisema: Kura ya maoni ya kujitenga Kurdistan inakabiliwa na kizingiti kikubwa na kuna uwezekano kwamba itasitishwa au kuakhirishwa.

Sisitizo la Masud Barazani, kiongozi wa eneo lenye utawala wa ndani la Kurdistan huko kaskazini mwa Iraq la kutaka kuitishwa kura ya maoni ya kujitenga eneo hilo linapingana na katiba ya Iraq na kupingwa hata na wakazi wa eneo hilo ambao wametangaza mara kwa mara kwamba, hawakubaliani na suala la kujitenga na Iraq. Mwaka 1917 na 2005 Wakurdi wa eneo hilo walichagua kubakia ndani ya Iraq moja na kuendelea kushikamana na katiba ya nchi hiyo. Kwa msingi huo eneo la Kurdistan ni sehemu ya ardhi ya Iraq inayoongozwa kwa mfumo wa utawala wa federali.

Katika upande wa kimataifa pia suala la kuitishwa kura ya maoni ya kujitenga Kurdistan huko Iraq linahesabiwa kuwa ni jitihada za kuigawa nchi hiyo na kinyume na kanuni na sheria za kimataifa.

Miongoni mwa vigezo muhimu vya muundo wa nchi mbalimbali duniani ni kuwa na jamii yenye kaumu na dini mbalimbali. Uchunguzi uliofanyika kuhusu suala la utaifa (nationalism) na muundo wa jamii kote duniani umeonesha kuwa, nchi 14 pekee duniani ndizo zisizokuwa na muundo wenye kaumu kadhaa au jamii yenye kaumu za waliowachache, na nchi hizo zinaunda asilimia 4 tu ya jamii ya watu kote duniani. Kwa msingi huo utaifa wa kaumu ya Kikurdi ambao Masud Barazani anaung'ang'ania kwa udi na uvumba si tiba mujarabu ya mashaka ya mwanadamu wa leo bali utazidisha taasubi na chuki za kidini, kikaumu na kikabila. Hivyo basi suala hilo linapingana na Azimio la la Haki za Binadamu na hati ya Umoja wa Mataifa na halitakuwa na matokeo ghairi ya vita, kubakia nyuma kiuchumi na kijamii na kukanyaga zaidi haki za kimsingi za binadamu.

Masud Barazani

Ni kwa kutilia maanani hayo yote ndipo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likatoa azimio likitangaza waziwazi upinzani wake dhidi ya kura ya maoni ya kujitenga eneo la Kurdistan huko kaskazini mwa Iraq.