Wafungwa wanawake wa Bahrain waanza mgomo wa kula
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i35265-wafungwa_wanawake_wa_bahrain_waanza_mgomo_wa_kula
Wafungwa wanawake katika jela moja nchini Bahran wameanza mgomo wa kula, kulalamikia ukandamizaji na hatua ya hivi karibu ya watawala wa Aal-Khalifa ya kuwawekea vizuizi vya kutembelewa na jamaa zao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 05, 2017 10:53 UTC
  • Wafungwa wanawake wa Bahrain waanza mgomo wa kula

Wafungwa wanawake katika jela moja nchini Bahran wameanza mgomo wa kula, kulalamikia ukandamizaji na hatua ya hivi karibu ya watawala wa Aal-Khalifa ya kuwawekea vizuizi vya kutembelewa na jamaa zao.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Haki na Demokrasia ya Bahrain (BIRD), vyombo vya usalama nchini humo vimeweka uzio wa kioo katika sehemu ya kuwatembelea wafungwa katika Gereza la Isa, ili kuzuia wafungwa hao kupeana mikono au hata kuwakumbatia watu wa familia zao wanapowazuru.

Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu nchini Bahrain yanasema kuwa, askari gereza wa Bahrain wamewabaka wanaharakati wawili wanaozuiliwa katika jela hiyo, Ibtesam al-Sayegh na Najah al-Sheikh. 

Wanawake wa Bahrain katika maandamano dhidi ya utawala wa Aal-Khalifa

Mwezi uliopita wa Septemba, mwanaharakati wa kisiasa nchini Bahrain Adel al-Gharif alisema jela za utawala wa Aal-Khalifa nchini Bahrain zimejaa watu wasio na hatia wakiwemo watoto 35 na wanawake 195.

Alisisitiza kuwa, makumi ya watu hao wanaoshikiliwa katika jela hizo, wanaugua maradhi mbalimbali kutokana na kunyimwa huduma za msingi, aghalabu yao wakipoteza maisha mara wanapoachiwa huru.

Katika hatua iliyozusha makelele ndani na nje ya nchi, watawala wa Manama kupitia Bunge mnamo mwezi Machi mwaka huu walipasisha sheria inayotaka kufunguliwa mashtaka raia katika mahakama za kijeshi nchini humo.