Serikali ya Iraq yapitisha vikwazo vipya dhidi ya eneo la Kurdistan
(last modified Tue, 10 Oct 2017 03:07:07 GMT )
Oct 10, 2017 03:07 UTC
  • Serikali ya Iraq yapitisha vikwazo vipya dhidi ya eneo la Kurdistan

Katika kujibu hatua ya viongozi wa eneo la Kurdistan ya Iraq ya kukiuka katiba na kuitisha kura ya maoni ya kutaka kujitenga na kujitangazia uhuru, serikali kuu ya Iraq imechukua maamuzi mapya ya kuliadhibu eneo hilo.

Shirika la Habari la Baghdad News limeripoti kwamba, taarifa iliyotolewa na ofisi ya Hider al-Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq kupitia kikao cha usalama wa taifa kilichohudhuriwa na waziri mkuu huyo imesema kuwa, hatua mpya za kinidhamu dhidi ya eneo hilo la Kurdistan ya Iraq tayari zimechukuliwa. Ripoti hiyo imesisitiza kuwa, hatua hizo hazitawahusu raia wa kawaida wa eneo la Kurdistan.

Masoud Barzani, kiongozi anayechochewa na Israe ili afanikishe njama ya kuigawa Iraq

Imezidi kufafanua kuwa, kipaumbele cha serikali ya Iraq kwanza ni kupambana na kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) na makundi mengine ya kigaidi na kadhalika kudhamini usalama na amani ya mipaka ya Iraq. Katika kikao hicho pia kumeamuliwa kwamba mitandao yote ya habari na mawasiliano yakiwemo mashirika ya simu, vitadhibitiwa na serikali kuu ya Baghdad kama ambavyo pia ofisi zake zitatakiwa kuhamishiwa mjini Baghdad. Kadhalika kikao hicho kimeitaka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Utruki kufanya mawasiliano yote kuhusiana na masuala ya mipaka na serikali kuu ya Iraq kama ambavyo pia nchi hizo jirani zimetakiwa kuendelea kufunga mipaka yao na eneo hilo la Kurdistan hadi serikali ya Baghdad itakapochukua udhibiti kamili wa mipaka hiyo.

Wakazi wa eneo la Kurdistan wakiwa wameshikilia bendera za utawala wa Kizayuni

Mbali na hayo serikali ya Iraq imeitaka Tehran na Ankara kuendelea kusimamisha miamala ya mauziano ya mafuta na eneo hilo na badala yake ziwasiliane na serikali kuu ya Baghdad tu. Hatua ya kuendeshwa kura ya maoni ya kutaka kujitenga eneo hilo iliyofanyika kinyume cha sheria hapo tarehe 25 mwezi jana kupitia kiburi cha Masoud Barzani, kiongozi wa Kurdistan, imeibua mgogoro katika mahusiano kati ya serikali kuu ya Baghdad na nchi za eneo pamoja na viongozi wa eneo hilo la Kurdistan.