Saad Hariri ajiuzulu uwaziri mkuu wa Lebanon akiwa safarini nchini Saudia
Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri ametangaza kujiuzulu wadhifa wake huo katika hotuba aliyotoa akiwa nchini Saudi Arabia.
Hariri ametangaza kujiuzulu katika taarifa aliyotoa kwa njia ya televisheni hii leo akitaja sababu kadhaa zilizomfanya achukue uamuzi huo wa ghafla ikiwemo hali ya usalama ndani ya Lebanon.
Aidha amedai kuwa anahisi kuna njama ya kutaka kumuua.
"Nimehisi wanataka kuniua, hivyo nimejiuzulu wadhifa wa uwaziri mkuu", ameeleza Hariri.
Ofisi ya Rais wa Lebanon Michel Aoun imetangaza kuwa Hariri alimpigia simu kiongozi huyo "kutokea nje ya Lebanon" kumtaarifu kuwa amejiuzulu na kwamba yeye Rais Aoun anamsubiri Hariri arejee nchini ili kusikia kutoka kwake kuhusu "hali na mazingira yaliyomfanya ajiuzulu".
Kujiuzulu kwa Hariri kumekuja chini ya mwezi mmoja baada ya yeye mwenyewe kutangaza mipango ya kuungana na Harakati ya Muqawama ya Lebanon Hizbullah kuunda serikali ya mseto.
Hata hivyo katika taarifa yake hiyo, Saad Hariri ameituhumu Hizbullah kwa kudai kwamba anapinga harakati hiyo kutumia silaha dhidi ya Walebanon na Wasyria. Aidha ameituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa inaingilia masuala ya nchi za Kiarabu za eneo ikiwemo Lebanon na kuongeza kwamba Hizbullah ni nguzo ya Iran katika eneo.
Hariri ametoa matamshi hayo ilhali Rais Michel Aoun wa Lebanon alishakanusha hapo kabla madai ya baadhi ya duru za Magharibi na za Kiarabu kwamba Iran inaingilia masuala ya ndani ya Lebanon na kueleza kwamba nchi yake hadi sasa haijashuhudia uingiliaji wowote wa Iran na kwamba madai yanayotolewa juu ya suala hilo hayana ukweli.
Kuhusiana na silaha za Muqawama wa Lebanon, Rais Aoun aidha amesema Hizbullah haitumii silaha zake katika uga wa ndani na kwamba silaha za harakati hiyo ya muqawama zinatumika kudhamini muqawama wa Walebanon tu katika kukabiliana na utawala wa Israel.
Wakati huohuo shakhsia mbalimbali wakiwemo wa kisiasa na kijeshi nchini Lebanon wamesema kujiuzulu Waziri Mkuu wa nchi hiyo Saad Hariri kumetokana na mashinikizo ya Saudi Arabia na kwamba utawala wa Riyadh haukuridhia kumruhusu kiongozi huyo hata atangaze uamuzi wake huo akiwa ndani ya nchi yake.
Hariri aliteuliwa kushika wadhifa wa uwaziri mkuu mwaka 2016 na aliwahi pia kushika wadhifa huo mwezi Novemba mwaka 2009 hadi Juni 2011.../