Yemen yazindua makombora mapya, Ansarullah yawaonya wavamizi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i36226-yemen_yazindua_makombora_mapya_ansarullah_yawaonya_wavamizi
Maafisa wa ngazi za juu wa Yemen na makamanda wa kijeshi wa harakati ya Ansarullah wamezindua makombora mapya yaliyotengenezwa nchini humo katika maoneyesho yaliyofanyika katika mji wa bandarini wa Hudaydah.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 07, 2017 14:15 UTC
  • Yemen yazindua makombora mapya, Ansarullah yawaonya wavamizi

Maafisa wa ngazi za juu wa Yemen na makamanda wa kijeshi wa harakati ya Ansarullah wamezindua makombora mapya yaliyotengenezwa nchini humo katika maoneyesho yaliyofanyika katika mji wa bandarini wa Hudaydah.

Saleh al-Sammad, Rais wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen ni kati ya maafisa ambao walitembelea maonyesho hayo ya makombora maalumu ya kutumiwa na jeshi la majini na gadi ya pwani.

Kamanda mmoja wa kijeshi amesema makombora hayo yenye uwezo wa hali ya juu ya kulenga shabaha yamepewa jina la Mandab 1 na yameundwa kikamilifu nchini Yemen.

Maonyesho hayo yamefanyika siku moja baada ya Jeshi la Yemen kutangaza kuwa lilillenga kwa mafanikio Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mfalme Khalid katika mji mkuu wa Saudia, Riyadh kwa kutumia kombora la Borkan H2. Shambulizi hilo lilitekelezwa katika fremu ya ulipizaji kisasi kufuatia hujuma za Saudia na waitifaki wake dhidi ya Yemen.

Wakati huo huo, msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ametoa onyo kali kwa nchi vamizi kuwa zisijaribu kufanya chokochoko yoyote katika pwani ya magharibi mwa nchi hiyo. Indhari hiyo imetolewa na Mohammad Abdulsalam, msemaji rasmi wa Ansarullah katika ukurasa wake wa Tweeter.

Uharibifu unaosababishwa na Saudia katika maeneo ya raia Yemen

Vita vya Saudia na waitifaki wake dhidi ya Yemen vilianzishwa mwezi Machi mwaka 2015 kwa kisingizio cha kutaka kumrejesha madarakani rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kuitoroka nchi Abd Rabbuh Mansur Hadi.

Vita hivyo vingali vinaendelea kwa mwaka wa tatu sasa bila ya utawala wa Aal Saud na waitifaki wake kufikia malengo haramu waliyokusudia. Watu zaidi ya 13,000 , wengi wakiwa ni wanawake na watoto, wameuawa katika hujuma hiyo ya Saudia nchini Yemen.