Chama cha Hariri: Hatutambui kujiuzulu Saad Hariri, anapaswa kurudi Lebanon haraka
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i36284-chama_cha_hariri_hatutambui_kujiuzulu_saad_hariri_anapaswa_kurudi_lebanon_haraka
Chama cha al-Mustaqbal kinachoongozwa na Saad al-Hiriri, Waziri Mkuu wa Lebanon aliyetangaza kujiuzulu wadhifa huo Jumamosi iliyopita huko Saudia, kimesema kuwa bado kinamtambua kuwa ni waziri mkuu wa Lebanon.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 09, 2017 13:50 UTC
  • Chama cha Hariri: Hatutambui kujiuzulu Saad Hariri, anapaswa kurudi Lebanon haraka

Chama cha al-Mustaqbal kinachoongozwa na Saad al-Hiriri, Waziri Mkuu wa Lebanon aliyetangaza kujiuzulu wadhifa huo Jumamosi iliyopita huko Saudia, kimesema kuwa bado kinamtambua kuwa ni waziri mkuu wa Lebanon.

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa chama cha al-Mustaqbal kupitia televisheni, mbali na kumtambua Saad Hariri kuwa bado ni Waziri Mkuu wa Lebanon, imemtaka arejee nchini humo haraka sana. Taarifa hiyo imebainisha kwamba, kurejea mwanasiasa huyo kutoka Saudia ni suala muhimu kwa ajili ya kuweka mambo sawa nchini Lebanon.

Saad Hariri

Nayo kwa upande wake, serikali ya Lebanon imetangaza leo kwamba, inaamini kuwa Saad Hariri anashikiliwa nchini Saudia kinyume na matakwa yake, na kwamba uwepo wake nchini humo ni kinyume cha sheria. Hayo yanajiri katika hali ambayo mapema leo Saudi Arabia imetoa taarifa ikiwataka raia wake wanaoishi Lebanon kuondoka nchini humo haraka. Kabla ya Saudia, serikali ya Bahrain ambayo nayo ni mshirika mkubwa wa Saudia ilikuwa imetoa tamko kama hilo, kwa kuwataka raia wake waishio Lebanon kuondoka nchini humo.

Mfalme Salman wa Saudia

Hatua ya chama cha al-Mustaqbal cha Hariri ya kutotambua kujiuzulu kwake na kumtaka arejee nchini Lebanon, inatathminiwa na weledi wa mambo kuwa ni pigo kwa utawala wa Aal-Saud ambao una nia ya kukishinikiza chama hicho na kukitwisha matakwa yake ili kuzusha mzozo wa kisiasa ndani ya Lebanon. Viongozi wa Lebanon wanaishutumu Saudia kwa kuingilia masuala yake ya ndani na kuchochea migogoro wa kisiasa nchini humo.