Imarati yakerwa na kuwasilishwa kesi dhidi yake ICC, yailaumu Qatar
(last modified Wed, 29 Nov 2017 08:12:42 GMT )
Nov 29, 2017 08:12 UTC
  • Imarati yakerwa na kuwasilishwa kesi dhidi yake ICC, yailaumu Qatar

Waziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu ameeleza kughadhibishwa kwa Imarati na hatua ya shirika moja la kutetea haki za binadamu kufungua faili la jinai za kivita za nchi hiyo dhidi ya Yemen.

Anwar Gargash ameandika kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, shirika hilo linalofahamika kama Arab Organization for Human Rights (AOHR) lenye makao makuu yake mjini London limeishtaki Imarati kwa niaba ya Qatar.

Ameandika kuwa: Shirika la AOHR, lenye anuani ya mawasiliano Qatar, limewasilisha kesi dhidi yetu katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. Watu wenye ufahamu wa mambo wanatambua kuwa mchezo huu wa kutaka kuibua makelele dhidi yetu ni wa Qatar.  

Watoto ndio wahanga wakuu wa kushambuliwa Yemen

Jumatatu iliyopita, shirika hilo liliituhumu Imarati kuwa imetenda jinai za kibinadamu dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen, kwa kutumia mabomu yaliyopigwa marufuku ya vishada sambamba na kuwakodi mamluki kuwaua na kuwatesa raia wa nchi hiyo maskini ya Kiarabu.

Saudia kwa uungaji mkono wa Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, Imarati na baadhi ya nchi za Kiarabu, ilianzisha mashambulizi ya kikatili ya pande zote dhidi ya wananchi wa Yemen mwezi Machi 2015, ambapo watu zaidi ya 12 elfu wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa.

Tags