EU: Hali ya Sheikh Issa Qassim wa Bahrain inatutia wasiwasi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i37055-eu_hali_ya_sheikh_issa_qassim_wa_bahrain_inatutia_wasiwasi
Umoja wa Ulaya umeelezea wasiwasi wake kutokana na hali mbaya ya kiafya Ayatullah Sheikh Issa Qassim, mwanachuoni mkubwa wa Bahrain aliyezingirwa kila upande na askari wa utawala wa Aal Khalifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 02, 2017 00:42 UTC
  • EU: Hali ya Sheikh Issa Qassim wa Bahrain inatutia wasiwasi

Umoja wa Ulaya umeelezea wasiwasi wake kutokana na hali mbaya ya kiafya Ayatullah Sheikh Issa Qassim, mwanachuoni mkubwa wa Bahrain aliyezingirwa kila upande na askari wa utawala wa Aal Khalifa.

Shirika la habari la Mehr limeunukuu Umoja wa Ulaya akisema katika taarifa yake ya jana Ijumaa kwamba, umoja huo unafuatilia kwa karibu hali hatari ya kiafya aliyo nayo Sheikh Issa Qassim nchini Bahrain.

Tamko hilo la Umoja wa Ulaya limesema, hatua zilizochukuliwa na serikali ya Bahrain dhidi ya Sheikh Issa Qassim zinakinzana na nasaha zilizotolewa na kamati huru ya kutafuta ukweli nchini humo na kwamba Umoja wa Ulaya unapendekeza kufanyika mabadiliko makubwa ya kimsingi nchini Bahrain kwa ajili ya kurejesha umoja wa kitaifa na utulivu.

Maandamano ya amani ya wananchi wanamapinduzi wa Bahrain

 

Umoja huo umeelezea kusikitishwa kwake na hatua ya ukoo wa kifalme wa Manama kumpokonya uraia Sheikh Issa Qassim mwezi Juni 2016 na kumfunga kifungo cha nyumbani tangu wakadi huo hadi hivi sasa. Umesisitiza kuwa, hatua hiyo inaongeza mivutano ya kikabila, mizozo na mifarakano nchini Bahrain. Aidha Umoja wa Ulaya umesema, unafuatilia kwa karibu matukio ya Bahrain na una una hamu ya kuona kunapatikana umoja wa kitaifa kwa njia za amani.

Kuanzia tarehe 14 Februari 2011, wananchi wanamapinduzi wa Bahrain walianzisha wimbi la kupinga utawala wa kiimla wa nchi hiyo na kutaka haki zao za kimsingi kama za kujichagulia wenyewe viongozi wao. Hata hivyo Saudi Arabia ilituma jeshi lake na kukandamiza maandamano ya amani ya wananchi wa nchi hiyo, ingawa jeshi hilo la Aal Saudilimeshindwa kuzima harakati hizo za wananchi wa Bahrain.