Rais wa Lebanon: Mgogoro uliozuka baada ya kujiuzulu Hariri umemalizika
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i37099-rais_wa_lebanon_mgogoro_uliozuka_baada_ya_kujiuzulu_hariri_umemalizika
Rais Michel Aoun wa Lebanon amesema: mgogoro uliojitokeza baada ya Saad Hariri kutangaza kujiuzulu uwaziri mkuu umemalizika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 02, 2017 23:13 UTC
  • Rais wa Lebanon: Mgogoro uliozuka baada ya kujiuzulu Hariri umemalizika

Rais Michel Aoun wa Lebanon amesema: mgogoro uliojitokeza baada ya Saad Hariri kutangaza kujiuzulu uwaziri mkuu umemalizika.

Aoun ameyasema hayo katika kikao cha siku tatu cha nchi zinazopakana na bahari ya Mediterania kilichofanyika mjini Rome, Italia kujadili uthabiti na usalama, uhajiri, mipaka na mapambano dhidi ya ugaidi.

Rais wa Lebanon amesisitizia kuhusu umuhimu wa kushikamana na umoja wa kitaifa na kuongeza kuwa mgogoro uliojitokeza nchini humo baada ya kujiuzulu Hariri umemalizika.

Katika upande mwengine afisa mmoja mwandamizi wa harakati ya muqawama ya Lebanon Hizbullah amesema Katibu Mkuu wa harakati hiyo Sayyid Hassan Nasrullah amemwandikia barua Waziri Mkuu wa nchi hiyo Saad Hariri akisisitizia uungaji mkono wake kwa Hariri katika hali zote.

Sayyid Hassan Nasrullah (kushoto) na Saad Hariri

Katika barua hiyo, Sayyid Hassan Nasrullah amesisitiza kuwa Hizbullah itashirikiana na Saad Hariri kwa ajili ya kuimarisha uthabiti ndani ya Lebanon, kuilinda serikali, maisha ya waziri mkuu huyo na kuzuia kutokea fitna nchini humo.

Hayo yanajiri katika hali ambayo duru za kisiasa zilizo karibu na Hizbullah zimekataa kuthibitisha wala kukanusha uwezekano wa Sayyid Hassan Nasrullah kukutana na kufanya mazungumzo na Saad Hariri.

Saad Hariri alitangaza kujiuzulu wadhifa wa uwaziri mkuu wa Lebanon tarehe 4 ya mwezi huu wa Novemba akiwa mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, lakini akatengua uamuzi wake huo tarehe 22 wakati aliporejea nchini Lebanon na baada ya safari yake katika nchi za Ufaransa na Misri.../