Baraza la Usalama kupigia kura muswada wa kulaani uamuzi wa Trump
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litachunguza muswada unaopinga uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kutambua rasmi Quds kuwa ni mji mkuu wa Israel.
Misri iliwasilisha muswada huo Jumamosi iliyopita katika Baraza la Usalama ikitaka kubatilishwa uamuzi huo wa upande mmoja wa Marekani.
Matini ya muswada huo ambayo haikutaja jina la Marekani moja kwa moja, imeeleza kusikitisha sana na uamuzi uliochukuliwa hivi karibuni kuhusu Quds na kusisitiza kuwa, hali ya mustakbali wa mji huo inapaswa kuainishwa kupitia njia ya mazungumzo.
Muswada huo pia unasisitiza kuwa, uamuzi wowote au hatua yoyote inayochukuliwa kwa shabaha ya kubadili sifa na muundo wa kijiografia wa mji wa Quds (Jerusalem) unakiuka sheria na unapaswa kupingwa.
Wanadiplomasia wanatazamia kuwa, muswada huo utakabiliwa na kura ya veto ya Marekani wakati utakapopigiwa kura hii leo katika Baraza la Usalama.
Mwaka 1980 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio linalosisitiza kuwa, hatua zote zinazochukuliwa na Isreal huko Quds na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina hazina itibari na hadhi yoyote.