Mgogoro wa Qatar unazidi kuwa mkubwa, Saudia yazidisha mashinikizo
Katika kile kinachoonekana ni kukosekana matumaini kabisa ya kutatuliwa mgogoro ulioanzishwa na Bani Saud dhidi ya Qatar, serikali ya kifalme ya Saudi Arabia imeamua kuufunga kikamilifu kivuko cha mpaka wake wa ardhini na Qatar ambacho ilikifungua kidogo wakati wa msimu wa Hija.
Kivuko hicho cha Salwa, ndicho cha mwisho cha nchi kavu kilichokuwa kinatoa fursa ndogo kwa wananchi wa Qatar kutoka nchini humo kupitia ardhini. Televisheni ya al Jazeera ya Qatar jana (Jumatano) iliwanukuu maafisa wa Idara ya Uhamiaji ya Saudi Arabia wakisema kuwa, viongozi wa nchi hiyo wamewaamrisha kukifunga kikamilifu kivuko cha Salwa.
Muda wa siku 14 uliotolewa na Saudia kwa raia wote wa Qatar kuondoka nchini humo ulimalizika mwezi Juni 2017. Hata hivyo kivuko cha Salwa kilifunguliwa wakati wa msimu wa Hija. Siku ya Jumatatu ya tarehe 5 Juni mwaka huu (2017), Saudia ilikuwa ya kwanza kukata uhusiano wake wote na Qatar na siku hiyo hiyo ikafuatiwa baadaye na Bahrain, Imarati na Misri kwa madai kuwa Doha inaingilia masuala ya ndani ya nchi hizo na pia ina uhusiano na makundi yaliyotajwa na nchi hizo nne kuwa ni ya kigaidi kama ambavyo ziliitaka pia ivunje uhusiano wake na Iran na pia Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, HAMAS.
Hata hivyo kitu ambacho inaonekana hakikufikiriwa na nchi hizo nne ni kwamba Qatar ingeliweza kuomba msaada kutoka kwa Iran ambayo kwa hakika ndilo kimbilio pekee walilobakishiwa wananchi wa Qatar. Inaonekana Saudia na nchi hizo tatu za Kiarabu zilikuwa na yakini kuwa zingeliisambaratisha mara moja Qatar hata hivyo zimefeli huku zikiwa zimeshatumia nyenzo zao zote.