Iran na Misri zatoa wito wa kuendelea kuungwa mkono Palestina
(last modified Tue, 09 Jan 2018 15:58:50 GMT )
Jan 09, 2018 15:58 UTC
  • Iran na Misri zatoa wito wa kuendelea kuungwa mkono Palestina

Hossein Amir-Abdollahian, msaidizi maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesisitizia umuhimu wa kuendelea kuungwa mkono kadhia ya Palestina.

Amir-Abdollahian amesema hayo leo katika mazungumzo na Yasser Othman, mkuu wa ofisi inayoshughulikia maslahi ya Misri mjini Tehran, ambapo ameashiria hatua ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuitangaza Beitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel na kusema kwamba, Quds ni mali ya Ulimwengu wa Kiislamu na nchi zote za Kiislamu na kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa pamoja na nchi nyingine za Kiislamu inapinga vikali kutekelezwa kivitendo kwa uamuzi huo wa Trump.

Amesema Iran daima imekuwa mtetezi wa haki za wananchi madhulumu wa Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu na itaendelea kufanya hivyo.

Tangazo la uhasama la Trump dhidi ya Quds limepingwa kote duniani

Mkurugenzi Mkuu wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa kadhalika amesisitizia udharura wa kuweko ushirikiano wa dhati na wa kivitendo wa kupambana na jinamizi la ugaidi.

Amir-Abdollahian na mwanadiplomasia wa ngazi za juu wa Misri aidha wamezungumzia masuala muhimu ya kieneo na kimataifa.

Chokochoko hiyo ya Rais Trump wa Marekani ya kuitangaza Beitul-Muqaddas kuwa mji mkuu wa Israel ilikabiliwa na malalamiko na maandamano katika pembe mbalimbali za dunia. 

Tags