Marekani yakosolewa kwa kuipunguzia msaada UNRWA
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia wakimbizi wa Kipalestina limekosoa vikali hatua ya Marekani ya kuipunguzia msaada tasisi hiyo kwa zaidi ya asilimia 50.
Chris Gunness, msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa UNRWA ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, uamuzi huo wa Marekani wa kulipunguzia msaada shirika hilo ni ya kutamausha na kwamba wakimbizi wa Kipalestina wanakodolewa macho na mgogoro mkubwa wa kibinadamu ambao haujawahi kushuhudiwa.
Amesema mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina ambao wamekuwa wakitegemea misaada ya UNRWA yumkini wakakosa huduma za msingi akisisitiza kuwa mwaka huu 2018 umeanza huku shirika hilo likikabiliwa na nakisi ya dola 174 za Marekani ya bajeti yake.
Kwa mujibu wa gazeti la Jordan la al-Ghad, wafanyakazi wasiopungua 100 wa UNRWA katika nchi hiyo walifutwa kazi, ikiwa ni katika taathira hasi ya Washington kuipunguzia taasisi hiyo msaada.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ametahadharisha kuwa, kupunguziwa msaada Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa kutapelekea wakimbizi wa Kipalestina wakose huduma za msingi kama vile elimu, afya na makazi.
UNRWA imekuwa ikitoa huduma mbali mbali kwa wakimbizi milioni tano wa Kipalestina katika eneo la Mashariki ya Kati.