Bunge la Iraq kuchukua uamuzi kuhusu tarehe ya kufanyika uchaguzi
Bunge la Iraq leo Jumamosi limeshindwa kufikia uamuzi kuhusiana na tarehe ya kufanyika uchaguzi wa Bunge katika kikao chake maalumu hivi leo.
Televisheni ya taifa ya Iraq imetangaza kuwa, baada ya kushindwa kufikiwa uamuzi kuhusiana na suala hilo, Salim al-Jabouri Spika wa Bunge la Iraq amewaita viongozi wa mirengo mbalimbali katika Bunge hilo kwenye kikao kitakachofanyika kesho Jumapili.
Kikao cha leo cha Bunge la Iraq ni cha tatu kuitishwa katika kipindi cha wiki moja kwa ajili ya kujadili na kufikia mwafaka kuhusiana na tarehe ya kufanyika uchaguzi wa Bunge.
Kabla ya hapo, Kamisheni Huru ya Uchaguzi na Baraza la Mawaziri lilikuwa limetangaza kuwa, uchaguzi wa Bunge utafanyika pamoja na ule wa Mabaraza ya Miji tarehe 12 Mei mwaka huu.
Hata hivyo, viongozi kadhaa wa mirengo ya Wakurdi na Ahlu Sunna Waljamaa wanataka uchaguzi huo usogezwe mbele kwa uchache miezi mitano mpaka sita mingine.
Hii ni katika hali ambayo, mrengo wa Mashia katika Bunge la Iraq umetangaza kuwa, katika Katiba ya Iraq hakuna kipengee kinachoelezwa kuakhirisha uchaguzi wa Bunge na kwamba, kufanya hivyo ni kukiuka wazi Katiba ya nchi.
Tayari Waziri Mkuu nchini Iraq, Haider al-Abadi ametangaza bayana kwamba, uchaguzi wa bunge la nchi hiyo utafanyika katika tarehe iliyopangwa ya 12 Mei mwaka huu na kwamba kamwe hautaahirishwa.