UNRWA yazindua mfuko wa kimataifa baada ya Marekani kuipungizia misaada
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i39359-unrwa_yazindua_mfuko_wa_kimataifa_baada_ya_marekani_kuipungizia_misaada
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa UNRWA limezindua mfuko wa kimataifa utakaoisaidia taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake baada ya Marekani kuipunguzia misaada.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 23, 2018 04:24 UTC
  • UNRWA yazindua mfuko wa kimataifa baada ya Marekani kuipungizia misaada

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa UNRWA limezindua mfuko wa kimataifa utakaoisaidia taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake baada ya Marekani kuipunguzia misaada.

Uzinduzi huo uliongozwa na Pierre Krähenbühl, Kamishna Mkuu wa UNRWA katika Ukanda wa Gaza jana Jumatatu.

Akihutubu katika hafla ya uzinduzi huo, Krähenbühl amewapa matumaini wakimbizi wa Kipalestina hususan watoto wadogo kuwa mambo yatatengamaa karibuni hivi na wataweza kuendelea na masomo na kupokea huduma za afya. 

Kampeni ya uzinduzi wa mfuko huo wa kimataifa inaendeshwa pia kwenye mitandao ya kijamii kupitia kaulimbiu #Hadhi Haina Thamani.

UNRWA imekuwa ikitoa huduma mbali mbali kwa wakimbizi zaidi ya milioni tano wa Kipalestina katika nchi za eneo la Mashariki ya Kati kama Syria, Lebanon na Jordan.

Watoto wakimbizi wa Kipalestina

Hivi karibuni, Chris Gunness, msemaji wa UNRWA aliliambia shirika la habari la AFP kuwa, uamuzi huo wa Marekani wa kulipunguzia msaada shirika hilo ni ya kutamausha na kwamba wakimbizi wa Kipalestina wanakodolewa macho na mgogoro mkubwa wa kibinadamu ambao haujawahi kushuhudiwa.

Pierre Krähenbühl, Kamishna Mkuu wa UNRWA ameongeza kuwa, kufuatia hatua ya Marekani kuipunguzia misaada taasisi hiyo, shule 700 za shirika hilo zenye wanafunzi zaidi ya laki 5 wa Kipalestina ziko katika hatari ya kufungwa, mbali na Wapalestina milioni 3 kukosa huduma za afya.