Mwanamfalme wa Bahrain atembelea Israel, atazamiwa kuhudhuria bunge
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i39955-mwanamfalme_wa_bahrain_atembelea_israel_atazamiwa_kuhudhuria_bunge
Waziri wa Mawasiliano wa utawala wa Kizayuni wa Israel Ayoub Kara amethibitisha kuwa amekutana na mwanamfalme wa Bahrain Mubarak Aal Khalifa mjini Tel Aviv.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 05, 2018 13:07 UTC
  • Mwanamfalme wa Bahrain atembelea Israel, atazamiwa kuhudhuria bunge

Waziri wa Mawasiliano wa utawala wa Kizayuni wa Israel Ayoub Kara amethibitisha kuwa amekutana na mwanamfalme wa Bahrain Mubarak Aal Khalifa mjini Tel Aviv.

Kara ameandika katika ukurasa wake wa kijamii wa Twitter: "Nimekutana kwa mara ya kwanza hadharani na Mubarak Aal Khalifa, mwanamfalme wa Bahrain ili kuimarisha uhusiano kati ya nchi zetu mbili". Waziri huyo wa Mawasiliano wa utawala wa Kizayuni wa Israel amejigamba kuwa mkutano huo ni ishara za kukua uhusiano wa Tel Aviv na Manama.

Ikumbukwe kuwa, hadharani, utawala wa Bahrain unaitangaza Israel kwamba ni adui yake wa jadi.

Ayoub Kara ameongeza kuwa, leo alitazamia kupata heshima ya kumkaribisha Mubarak Aal Khalifa katika bunge la Israel, Knesset. Waziri huyo wa Mawasiliano wa utawala wa Kizayuni ameweka pia katika ukurasa wake wa Twitter picha ya pamoja aliyopiga na mwanamfalme huyo wa Bahrain.

Ayoub Kara (kushoto) katika picha ya pamoja na Mubarak Aal Khalifa

Nchi za Kiarabu zimekuwa zikijionyesha kuwa ni maadui wa Israel na waungaji mkono wa mapambano ya Wapalestina dhidi ya uvamizi na ukaliwaji wa mabavu wa ardhi zao unaofanywa na utawala huo ghasibu.

Hata hivyo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekiri kuwa utawala huo haramu una mfungamano na ulimwengu wa Kiarabu na kwamba uhusiano wa pande hizo mbili umo katika hali ya kustawi.

Mwaka uliopita vyombo vya habari viliripoti kuwa ujumbe wa Bahrain uliwasili huko Israel kufikisha salamu maalumu kutoka kwa mfalme wa nchi hiyo.

Mnamo mwaka 2016, Bahrain ilikuwa nchi pekee ya Ghuba ya Uajemi ambayo iliomboleza hadharani kifo cha aliyekuwa rais wa utawala haramu wa Kizayuni Shimon Peres.../