Madai ya James Mattis dhidi ya Iran katika kuikingia kifua Israel
Waziri wa Ulinzi wa Marekani akiwa na lengo la kutetea uvamizi wa utawala haramu wa Israel huko Syria na dhidi ya mhimili wa muqawama amedai kwamba, Iran ndio tatizo kubwa katika Mashariki ya Kati.
James Mattis amedai kwamba, eti Iran ndio kikwazo na tatizo kubwa kwa Marekani na Israel katika Mashariki ya Kati.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani ameonyesha hasira zake dhidi ya Syria, Iraq, Lebanon na Yemen na kuituhumu Iran kwamba, eti imekuwa ikivuruga amani na usalama wa Mashariki ya Kati.
Matamshi hayo ya James Mattis bila shaka yalikuwa na lengo la kuhalalisha uvamizi wa hivi karibuni wa ndege za kijeshi za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya ardhi ya Syria.
Hivi karibuni serikali ya Marekani imetoa taarifa rasmi ambapo sambamba na kuunga mkono uvamizi wa Israel dhidi ya Syria, imeonyesha kukasirishwa kwake mno na ushirikiano uliopo baina ya Iran na Syria katika kukabiliana na makuandi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Washington na Tel Aviv.
Kikosi cha ulinzi wa anga cha jeshi la Syria siku ya Jumamosi ya tarehe 10 Februari kiliitungua na kuiangusha ndege ya kivita aina ya F16 ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel iliyovamia anga ya nchi hiyo.
Kutunguliwa ndege hiyo ya kijeshi ya Israel kumethibitisha kwamba, madai ya utawala huo ya kutaka kuwaonyesha walimwengu kwamba, utawala huo ghasibu una jeshi la kisasa kabisa la anga katika Mashariki ya Kati ni ya uongo na hadaa tupu.