Kugawanywa Yemen, ajenda ya Saudia na Imarati
Waziri MKuu wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen alisema siku ya Alkhamisi kwamba Saudi Arabia na Umoja wa Falame za Kiarabu zina nia ya kuigawa Yemen katika sehemu mbili na kisha kuiunganisha nchi hiyo na ardhi za nchi hizo mbili vamizi.
Abdulaziz bin Habtou amesema Saudia ina mpango wa kutaka kutwaa kaskazini mwa Yemen nayo Imarati kusini mwa nchi hiyo masikini ya Kiarabu. Matukio ya eneo yanathibitisha wazi kwamba kubadilishwa Yemen kuwa uwanja wa mashindano ya wachokozi na wavamizi yana matokeo hatari kwa Yemen na kwa eneo zima la Mashariki ya Kati, yakiwemo ya kugawanywa nchi hiyo katika maeneo kadhaa yasiyo na utawala mmoja. Saudi Arabia na Imarati tayari zimekubaliana kushirikiana katika kudhibiti na kutawala maeneo tofauti ya Yemen. Kwa mujibu wa makubaliano hayo Saudia ina mpango wa kudhibiti maeneo ya kaskazini mwa Yemen hadi kufikia mji mkuu Saaa nayo Imarati idhibiti maeneo na mikoa yote ya kusini mwa nchi hiyo.
Kwa msingi huo nchi mbili hizo vamizi ziko mbioni kutekeleza mipango ya kubaili miundo ya kijamii katika maeneo ya udhibiti wao na vilevile kuanzisha vituo vyao vya kijeshi katika maeneo hayo. Uchunguzi wa baadhi ya mienendo ya kieneo ya Imarati unathibitisha wazi kwamba nchi hiyo licha ya kujiepusha kugongana moja kwa moja na Saudia inatekeleza mikakati ya siri ya kuimarisha ushawishi wake katika nchi za Kiarabu na hivyo kutoachwa nyuma na mshindani wake katika eneo, Saudia. Licha ya kuwa nchi mbili hizo zinashirikiana kikamilifu katika medani ya vita dhidi ya Yemen lakini zinatofautiana pakubwa katika uwanja wa siasa zao nchini humo, jambo ambalo limekuwa likionekana waziwazi katika mikwaruzano na tamaa yao kupora ardhi ya Yemen.
Kuhusiana na hilo, Khalil al-Miqdad, mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema: Saudi Arabia na Imarati ndio wahusika wakuu wa hali ya hivi sasa ya Yemen kwa sababu ndio wanaofanya juhudi za kuidhibiti nchi hiyo. Hata hivyo hali ya mambo nchini humo imetoka kwenye udhibiti wao.
Matokeo ya pekee ya vita vya watawala wa Kiarabu kwa watu wa Yemen yamekuwa ni mauti, magonjwa, ukimbizi na kuharibiwa nchi yao. Tawakkul Karman, mwanaharakati wa Yemen na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel pia anasisitiza kwamba Saudi Arabia na Imarati zinatumia ujanja na hadaa kwa lengo la kuwaangamiza Wayemen, kuaharibu miundombinu ya nchi hiyo pamoja na kupora utajiri wake. Anazihutubu nchi hizo vamizi ambazo zinadai kuwa zimeiingia nchini humo kwa lengo la kuwaokoa Wayemen kwa kusema: ' Nyinyi mnafanya juhudi za kugawa na kuifanya Yemen kuwa nchi ndogo ili mpate kufuatilia siasa zenu za ubeberu nchini humo.'
Tokea tarehe 26 mwezi Machi 2015 Saudi Arabia na washirika wake wamekuwa wakiendesha vita vya uvamizi nchini Yemen kwa madai ya kutaka kuirejesha madarakani serikali ya zamani ya nchi hiyo iliyojiuzulu na kuikimbia nchi.
Uingiliaji unaoongezeka kila leo wa Saudi Arabia na Imarati huko Yemen unapaswa kuchunguzwa katika mtazamo wa tamaa ya muda mrefu ya watawala wa Kiarabu na hasa wa ukoo wa Aal Saud na Aal Nahyan pamoja na washirika wao wa nchi za Magharibi, ya kutaka kuidhibiti Yemen kwa malengo ya kistratijia. Hatua na njama ya Saudia na Imarati ya kutaka kuigawa Yemen katika maeneo kadha ya udhibiti wao, inatekelezwa katika hali ambayo katika miaka ya hivi karibuni nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zimekuwa zikitekeleza njama nyingine ya kutaka kuzigawa nchi za Mashariki ya Kati chini ya anwani tofauti kama 'Mashariki ya Kati Mpya.' Kwa msingi huo, suala hilo linadhihirisha wazi hatari ya njama zinazotekelezwa na maadui dhidi ya Yemen.