Feb 23, 2018 02:30 UTC
  • Aal Saud na jinamizi la ukosefu wa usalama

Vyombo vya habari ukiwemo mtandao wa Middle East Eye vimefichua kwamba, sababu ya kupelekwa idadi kubwa ya askari wa Pakistan nchini Saudi Arabia ni kulinda kizazi cha na ukoo wa mfalme wa nchi hiyo baada ya mageuzi na mapinduzi baridi yaliyofanyika ndani ya utawala wa kifalme na kuongezeka wasiwasi na hatari inayotishia watawala wa sasa.

Siku chache zilizopita Pakistan ilitangaza kuwa, itatuma askari wapya elfu moja nchini Saudi Arabia lakini hadi sasa kunaulizwa maswali mengi kwamba askari hao watakwenda kufanya nini na kwa nini wametumwa katika nchi hiyo. Waziri wa Ulinzi wa Pakistan ameliambia Baraza la Seneti la nchi hiyo kwamba kwa sasa Pakistan ina askari 1600 nchini Saudi Arabia. Jeshi la Pakistan limetangaza kuwa, askari wapya watakaotumwa Saudia watakuwa na jukumu la kutoa ushauri na kutoa mafunzo na kudai kuwa, hawatapelekwa nje ya mipaka ya nchi hiyo hususan huko Yemen. Miaka mitatu iliyopita pia Pakistan ilikataa kutuma askari wake nchini Yemen kushiriki katika mashambulizi ya Saudia dhidi ya watu wa nchi hiyo.

Mchambuzi Kamal Allam ambaye ni mwanachama wa taasisi ya Royal United Services Institute ya Uingereza anasema: "Inaonekana kuwa Wasaudi Arabia wana wasiwasi kuhusu hali ya ndani ya nchi hiyo na hawawaamini majirani na nchi zinazowazunguka, kwa msingi huo wameamua kuwafuata Wapakistan." Hii si mara ya kwanza kwa askari wa Pakistan kupelekwa nchini Saudi Arabia kulinda kizazi cha watawala wa kifalme wa nchi hiyo. Miaka ya mwanzoni mwa muongo wa 1970 Mfalme Faisal na Waziri Mkuu wa wakati huo wa Pakistan, Zulfikar Ali Bhutto walianzisha uhusiano mkubwa baina ya pande hizo mbili ambapo askari wa Pakistan walipelekwa Saudi Arabia. Mwaka 1982 pia kufuatia ombi la Mfalme Fahad, Rais wa wakati huo wa Pakistan Muhammad Zia-ul-Haq alituma kikosi cha jeshi nchini Saudi Arabia ambacho kilikuwa na jukumu la kulinda ukoo wa utawala wa kifalme wa nchi hiyo. Hivi sasa kikosi cha jeshi la Pakistan kilichotumwa Saudi Arabia pia kitatumiwa katika gadi maalumu ya kumlinda Muhammad bin Salman, ambaye ni mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo na kuimarisha ulinzi wa kizazi cha Aal Saud. 

Askari zaidi wa Pakistan kupelekwa Saudia

Itakumbukwa kuwa, miezi michache iliyopita maafisa wa utawala wa kifalme wa Saudia hususan mrithi wa kiti cha ufalme, Muhammad bin Salman walitumia fagio la chuma ndani ya ukoo wa kifalme na baina ya wafanya biashara wakubwa nchini humo kwa kisingizio cha kile kilichotajwa ni kupambana na ufisadi na kuwatia nguvuni makumi ya matajiri na wanasiasa wasiokubaliana na siasa za mrithi kijana wa ufalme wa nchi hiyo. Kwa msingi huo hatua ya mtoto wa Mfalme Salman ya kuunda kikosi kipya cha gadi ya mfalme kinachowashirikisha askari na wanajeshi wa nchi za kigeni ni ishara ya kutokuwa na imani na kikosi cha sasa cha gadi ya ukoo wa kifalme cha nchi hiyo.

Kutokana na mgawanyiko uliotokea katika kizazi cha Aal Saud baada ya hatua iliyochukuliwa na mfalme wa nchi hiyo ya kudhibiti madaraka zaidi kwa kuwaengua baadhi ya wapinzani wake na kuwafunga makumi ya wanamfalme na wafanya biashara wakubwa, hatua ambayo imezusha vita vipya vya kugombea madaraka nchini Saudi Arabia, watawala wa sasa wa nchi hiyo wameingiwa na wasiwasi kuhusu radiamali na jibu linaloweza kutolewa na wapinzani wao. Wakati huo huo watawala wa Riyadh wamezidisha ukandamizaji dhidi ya wananchi wanaopinga sera za kidikteta za ukoo wa kifalme na siasa za kuhodhi na kupora utajiri wa nchi hiyo. Kazi hii ya kudhibiti na kunyamazisha raia na wapinzani wa utawala wa kifalme inafanywa kwa kutumia majeshi na askari wa nchi za kigeni.

Mfalme wa Saudi Arabia

Sambamba na hayo, huko nje ya nchi utawala wa kifalme wa Saudi Arabia umeendeleza sera za kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine, na mfano hai wa ukweli huo ni mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudia na washirika wake dhidi ya watu wa Yemen na kutumwa askari wa nchi hiyo huko Bahrain kwenda kukandamiza harakati ya kupigania uadilifu na demokrasia nchini humo. 

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, sera za Aal Saud zinaonesha kuwa, utawala wa Riyadh umeshindwa kudhamini hata usalama na amani kwa kizazi cha ukoo wa kifalme licha ya kutenga bajeti lukuki ya mabilioni ya dola kwa ajili ya sekta ya ulinzi na usalama. Siasa hizo zisizo sahihi zinaendelea kuzusha mtengano baina ya watawala hao na raia wao na kuzidisha malalamiko ya wananchi. Hali hii kwa upande wake inazidisha jinamizi la usalama kwa watawala wa Riyadh na kuwafanya tegemezi zaidi kwa madola ya kigeni.             

Tags