Michel Aoun: Lebanon iko tayari kujilinda iwapo itashambuliwa na Israel
Rais wa Lebanon amesisitiza kuwa nchi hiyo imejiandaa kikamilifu kujilinda iwapo itashambuliwa na Israel.
Rais Michel Aoun amebainisha kuwa Lebanon inasisitiza suala la kuendelezwa amani na uthabiti katika mipaka yake ya kusini. Rais wa Lebanon aliyasema hayo jana Jumatatu huko Beirut mji mkuu wa nchi hiyo katika mazungumzo yake na Jean Pierre Lacroix Mjumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Udumishaji Amani pamoja na ujumbe aliofuatana nao.
Rais Aoun kwa mara nyingine tena ameukosoa utawala wa Kizayuni kwa kukiuka azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa na hatua ya utawala huo ya kukiuka anga ya Lebanon kwa ajili ya kuishambulia Syria.
Rais wa Lebanon jana alitembelea makao makuu ya komandi ya jeshi na kufanya mazungumzo na Jenerali Joseph Aoun Kamanda wa Jeshi la Lebanon. Mazungumzo kati ya pande mbili hizo yaligusia pia hali ya usalama wa nchi, utendaji wa jeshi na mahitaji ya jeshi hilo la taifa. Rais Michel Aoun amepongeza jitihada za jeshi la nchi hiyo katika kulinda uthabiti na kudumisha ulinzi nchini mkabala na chokochoko za utawala wa Kizayuni na kutilia mkazo suala la kuweko msimamo wa pamoja baina ya viongozi wa Lebanon na wananchi katika kuliunga mkono jeshi katika kulinda mipaka ya nchi kavu na baharini na maliasi za mafuta za nchi hiyo.
Itakumbukwa kuwa hivi karibuni Avigdor Lieberman Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni alidai kuwa machimbo nambari tisa ya mafuta na gesi ya Lebanon ni milki ya utawala huo; madai yaliyokabiliwa na radiamali kali ya viongozi wa Lebanon. Lebanon pia imejibu madai hayo ya Lieberman ikisema kuwa haitasalimu amri kwa vyovyote mbele ya haki yake hiyo ya mafuta.