Vita vipya vya maneno kati ya Saudi Arabia na Qatar
(last modified Sat, 10 Mar 2018 08:04:30 GMT )
Mar 10, 2018 08:04 UTC
  • Vita vipya vya maneno kati ya Saudi Arabia na Qatar

Vita vya maneno baina ya viongozi wa Qatar na Saudi Arabia kwa mara nyingine tena vimeshika kasi na kugonga vichwa vya habari.

Katika hali ambayo kumeripotiwa habari kuhusiana na upatanishi wa Marekani baina ya Qatar na Saudia Arabia, na kwa kuzingatia aina ya uhusiano wa Riyadh na Doha kwa Washington ambao ni wa aina fulani ya utegemezi, ilikuwa ikitarajiwa kwamba, mzozo baina ya nchi hizo mbili za Kiarabu ungechukua mkondo wa kushuka na kupooza. Mvutano huo ulianza Juni 5 mwaka jana na baada ya safari ya Rais Donald Trump wa Marekani huko Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia.

Matamshi ya Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia aliyoyatoa huko Cairo Misri, kwa mara nyingine tena yalichochea mzozo huo na kuufanya ushadidi tena. Akiwa huko, Bin Salman aliitaja Qatar kama 'nchi ndogo' na kwamba, mgogoro wa Qatar ni suala dogo ambalo halina umuhimu. Aidha alisema kwamba, waziri yeyote wa serikali ya Saudia anaweza kuupatia ufumbuzi mgogoro huo. 

Mgogoro wa Qatar na nchi nne za Saudia, Imarati, Misri na Bahrain

Katika radiamali yake kwa matamshi hayo, Muhammad bin Abdul-Rahman, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar alisema kuwa, kinyume na madai ya viongozi wa Saudia, utawala wa Riyadh umeshughulishwa mno na faili la Qatar. Qatar ni nchi ndogo lakini ina akili na tunawaheshimu na kuwapa umuhimu raia na watu wanaoishi katika nchi yetu.

Katika ada za mataifa, wakati 'utovu wa kisiasa' unapochukua nafasi ya 'mazungumzo ya kidiplomasia' katika matamshi ya viongozi, basi hubainisha kiwango cha hasira na ghadhabu za nchi husika. Hapana shaka kuwa, kile ambacho alikisema Muhmmad bin Salman akiwa nchini Misri kuhusiana na Qatar ni kielelezo cha wazi kwamba, Riyadh imekasirishwa mno na kuendelea mgogoro wa Qatar. Katika upande mwingine, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar sambamba na kusema kwamba, 'Saudia imeshughulishwa mno na faili la Qatar kutokana na kuwa, daima katika vikao na mikutano yote imekuwa ikitoa matamshi kuhusiana na Qatar', ameikumbusha Riyadh kuwa, hatua yake ya kujihusisha na faili la Doha ni kwa kiasi gani inaonyesha ilivyokasirishwa na suala la kuendelea mgogoro wa Qatar.

Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia

Nukta nyingine ni hii kwamba,  viongozi wa Doha na Riyadh katika matamshi na vita vyao vya maneno hivi karibuni kila mmoja amejaribu kulenga udhaifu wa mwenzake. Udhaifu muhimu zaidi wa Qatar ni kuwa kwake nchi ndogo ambayo ina masafa madogo na watu wachache. Qatar ina wakazi takribani milioni mbili na laki mbili ambapo moja ya saba kati yao  hawana asili ya Qatar. Aidha Qatar ina ukubwa wa kilomita mraba 11,586 na hivyo kuhesabiwa kuwa miongoni mwa nchi ndogo Mashariki ya Kati na ulimwenguni kwa ujumla.  Kwa kuzingatia kwamba, Qatar ipo baina ya nguvu mbili kubwa Mashariki ya Kati yaani Iran na Saudia, udhaifu huo unahisika zaidi.

Hata kama Bin Salman alifanya juhudi za kukumbushia udhaifu na mapungufu hayo na hivyo kwa namna fulani kuidunisha Qatar, lakini katika upande mwingine matamshi yake yalionyesha kwamba, hadi sasa Riyadh haiko tayari kufanya mazungumzo na Qatar kama nchi inayojitawala na yenye mamlaka. Kwa maneno mengine ni kuwa, Saudia ingali inaitazama Qatar kwa jicho la dharau au la Bwana kwa mtumwa au la mkubwa kwa mdogo. Hii ni katika hali ambayo, sababu hasa ya kuendelea mzozo baina ya Qatar na Saudia pamoja na nchi tatu za Imarati, Bahrain na Misri zilizoamua kufuata mkondo huo wa Riyadh ni hatua ya Doha ya kupinga kuburuzwa na kuamrishwa na  Saudia.

Muhammad bin Abdulrahman Al Thani, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar

Katika upande mwingine, Muhammad bin Abdul-Rahman, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar amelitaja suala la kutokomaa kisiasa viongozi wa sasa wa Saudia na ukiukaji wa haki za binadamu kwa raia wa nchi hiyo na wale wa kigeni kama nukta mbili hasi na dhaifu za Saudia. Sisitizo la Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar kwamba, Doha ina viongozi wenye akili, linaungwa mkono na matamshi na mitazamo inayoonyeshwa na viongozi wa Riyadh ambayo inabainisha wazi kutokomaa kwao kisiasa na hata kutokuwa na tadbiri ya kisiasa. Udhaifu huo unashuhudiwa katika serikali ya Saudia kiasi kwamba, Joaan bin Hamad bin Khalifa Al Thani kaka wa mfalme wa Qatar na mkuu wa kamati ya olimpiki ya nchi hiyo amemfananisha Muhammad bin Salman na Abu Jahal. Katika upande mwingine, ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya raia wa Saudia na wa kigeni wanaoishi Saudia ni mkuubwa kiasi kwamba, hivi sasa moja ya malalamiko makuu ya wananchi wa Uingereza dhidi ya safari ya Muhammad bin Salman huko London ni ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Aal Saud.

Kwa kuzingatia vita hivi vya maneno ambavyo matokeo yake ni kuibuka utovu na kuvunjiana heshima ya kisiasa tunaweza kusema kuwa, mzozo baina ya Qatar na Saudia utaendelea na hakuna matarajio ya kupatiwa ufumbuzi mgogoro huo katika kipindi cha muda mfupi ujao.

Tags