Hizbullah: Wanaowaua raia wa Yemen, hao ndio Mahitler wa zama hizi
Naibu Mkuu wa Baraza Kuu la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon amesema, anayehusika na jinai dhidi ya wanawake na watoto wa Yemen, huyo ndiye Hitler wa zama hizi; si Iran ambayo imezisaidia Iraq na Syria kukabiliana na kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh.
Sheikh Nabil Qaouk ametoa kauli hiyo kujibu matamshi ya kifedhuli yaliyotolewa hivi karibuni na mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Muhammad bin Salman, amedai kuwa Saudia inakabiliwa na changamoto katika eneo na duniani kwa jumla zinazosababishwa na Iran na makundi ya kigaidi. Mrithi huyo wa ufalme wa Saudi Arabia alitoa matamshi hayo siku ya Alkhamisi mjini Washington, Marekani katika mazungumzo na waziri wa ulinzi wa nchi hiyo James Mattis.
Sheikh Qaouk amebainisha kuwa, wao waliosababisha kuwepo dimbwi la damu nchini Yemen ndio "Mahitler wa zama hizi na Mahitler wa Kiarabu"; kwa sababu laiti kama si msaada na kujitolea mhanga kwa Iran, Daesh ingekuwa imeshazihodhi nchi za kandokando ya Ghuba ya Uajemi na kuweza kufika hata ndani ya nchi za Ulaya.
Mjumbe huyo wa Baraza Kuu la Utendaji la Hizbullah ameashiria pia hatua ya Saudia ya kuingilia uchaguzi wa bunge wa Lebanon kwa kuandaa orodha ya wagombea inaowaunga mkono ili kukabiliana na Hizbullah kwa madhumuni ya kubadilisha mlingano wa kisiasa ndani ya nchi hiyo na kufidia kushindwa kwake katika nchi za Iraq, Yemen na Syria na akasisitiza kwamba: vyovyote vile watakavyojitahidi kufanya hawatoweza kuubadilisha hata chembe mlingano wa kisiasa ndani ya Lebanon.
Sheikh Nabil Qaouk aidha amesema: Wasaudi wameanza kufanya maandalizi ya kutekeleza mpango wa Marekani uitwao "Mapatano ya Karne" na kulipigia upatu suala hilo la kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.../