Ndege za kivita za Saudia zaua watoto, wanawake Wayemeni mkoani Sa'ada
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i42028-ndege_za_kivita_za_saudia_zaua_watoto_wanawake_wayemeni_mkoani_sa'ada
Ndege za kivita za Saudia Arabia zimedondosha mabomu katika maeneo ya raia ya mkoa wa Sa'ada kaskazini mwa Yemen na kuua na kujeruhi raia 17 wakiwemo wanawake na watoto.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Mar 22, 2018 11:28 UTC
  • Ndege za kivita za Saudia zaua watoto, wanawake Wayemeni mkoani Sa'ada

Ndege za kivita za Saudia Arabia zimedondosha mabomu katika maeneo ya raia ya mkoa wa Sa'ada kaskazini mwa Yemen na kuua na kujeruhi raia 17 wakiwemo wanawake na watoto.

Kwa mujibu wa televisheni ya al-Masirah ya Yemen, ndege hizo za Saudia zilidondosha mabomu katika nyumba za raia wilayani Ghamar mapema leo Alhamisi.

Tukio hilo limejiri siku moja tu baada Jeshi la anga la Yemen kwa kushirikiana na harakati ya wananchi ya Answarullah kuitungua ndege ya kivita ya  Saudia katika mji wa Saada.

Baada ya kuangamizwa ndege hiyo ya kivita ya Saudia aina ya F-15 iliyoundwa Marekani, Ibrahim al-Shami, kamanda wa jeshi la anga ya Yemen amesema kuwa, ushindi mbalimbali wa Wayemen dhidi ya mvamizi huyo, utaendelea. 

Uharibifu unaotekelezwa na ndege za kivita za Saudia katika maeneo ya kiraia Yemen

Inafaa kuashiria kuwa hadi sasa jeshi la anga la Yemen kwa kushirikiana na harakati ya Kiislamu ya Answarullah, imeshaangamiza idadi kadhaa ya ndege za kivita za adui mvamizi wa Saudia. Saudia kwa kushirikiana na Marekani na utawala haramu wa Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu washirika wake, ilianzisha mashambulizi ya kila upande dhidi ya taifa masikini la Yemen hapo mwezi Machi 2015, ambapo mbali na uvamizi huo inatekeleza pia mzingiro wa ardhini, baharini na angani dhidi ya watu wa nchi hiyo. Lengo la uvamizi huo wa kinyama wa Saudia dhidi ya Yemen, lilitajwa kuwa ni kwa ajili ya kumrejesha madarakani kibaraka wake Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu wadhifa huo na kisha kutoroka nchi. Hata hivyo njama hizo za Saudia hazijaweza kufikia malengo hayo, ghairi ya kusababisha maafa ya maelfu ya raia wa Yemen na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa.