Malengo ya safari ya Amiri wa Qatar nchini Russia
Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, Amiri wa Qatar amefanya safari nchini Russia na kukutana na Rais Vladmir Putin wa nchi hiyo ambapo wamezungumzia masuala mbalimbali.
Safari ya Tamim bin Hamad mjini Moscow, imetajwa kuwa na umuhimu kwa mitazamo kadhaa. Kwanza ni kwamba safari hiyo imefanyika sambamba na safari kama hiyo ya Mohammad Bin Salman Al Saud, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia nchini Marekani. Ukweli ni kwamba, kuimarishwa uhusiano wa Saudia na Marekani ni sababu pia ya kuimarishwa uhusiano wa Qatar na Russia. Matukio hayo yamejiri sambamba na kushtadi mgogoro ndani ya nchi za Kiarabu, yaani kati ya Qatar na nchi nne za Kiarabu za Saudia, Imarati, Bahrain na Misri.
Aidha kuongezeka uhusiano wa Riyadh na Washington, kulikoenda sambamba na kupigwa kalamu nyekundu Rex W. Tillerson, waziri wa mambo ya nje wa zamani wa Marekani, ni ujumbe muhimu kwa Qatar kwamba serikali ya Marekani imefungamana zaidi na Saudia katika mgogoro huo kuliko wakati mwingine wowote. Kwa msingi huo suala la Doha kuimarisha mahusiano yake na Moscow ni jambo ambalo linapewa umuhimu mkubwa na Qatar. Katika uwanja huo alipokutana na Rais Vladmir Putin, Amiri wa Qatar alisema: "Tunaimani kuwa marafiki wetu wa Russia wako pamoja na sisi. Katika masuala ya ulimwengu wa Kiarabu, Russia imekuwa na nafasi chanya." Kwa ibara nyingine ni kwamba, Qatar si tu kwamba imevuka mashinikizo yanayotokana na siasa za uhasama za Saudia na nchi tatu nyingine za Kiarabu, bali ni kwamba inakusudia kulinda nafasi yake katika eneo la Mashariki ya Kati na ikiwezekana kupanua zaidi nafasi hiyo.
Ama umuhimu wa pili wa safari ya Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani mjini Moscow, unahusiana na uwepo wa kambi kadhaa ndani ya eneo la Mashariki ya Kati. Hii ni kusema kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya hivi karibuni, sambamba na Uturuki kukaribiana na Russia na pia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kumezaliwa kambi ya pembe tatu yaani Moscow, Ankara na Tehran kutokana mabadiliko ya eneo hilo. Migogoro ndani ya nchi za Kiarabu kwa upande mmoja imepelekea Qatar ijitenge na kambi ya Kiarabu, Israel na Magharibi. Ama kwa upande mwingine ni kwamba hatua ya kukaribiana mahusiano ya Uturuki na Qatar ambayo yanachangiwa pia na suala la uungaji mkono kwa harakati ya Ikhwanul Muslimin, na kadhalika uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki kwa Doha katika mzozo wa ndani ya nchi za Kiarabu, ni mambo ambayo yameishawishi Qatar kuegemea upande wa kambi hiyo ya Moscow, Tehran na Ankara.
Kwa msingi huo, mrengo mpya wa kisiasa unaozishirikisha nchi tatu zilizotajwa pamoja na Qatar kwa upande mwingine, utapelekea kushuhudiwa Mashariki ya Kati mpya kwa kuibuka kambi ya kisiasa ambayo itapunguza nguvu ya mfumo wa Kimarekani na Kimagharibi katika eneo hili. Moja ya matokeo hasi ya mfumo huo ni kuzuka mizozo kama ya Syria na Yemen ambayo inatokana na njama za baadhi ya nchi za Kiarabu, madola ya Magharibi na utawala wa Kizayuni. Hata kama Saudia inaungwa mkono kwa pande zote na Marekani na Uingereza, lakini haitoweza kufurukuta mbele ya pande nne za Uturuki, Iran, Russia na Qatar. Umuhimu mwingine wa safari ya Sheikh Tamim bin Hamad Al Than mjini Moscow, ni mikataba ya mauziano ya silaha iliyowekwa kati ya pande mbili.
Katika uwanja huo, mwezi Januari mwaka huu, balozi wa Qatar mjini Moscow alinukuliwa akisema kuwa serikali ya Doha inakusudia kununua ngao ya makombora aina ya S400 kutoka Russia. Makubaliano hayo yana maana kwamba kwa upande mmoja mbali na Moscow kufuatilia malengo yake ya kisiasa nchini Qatar, inafuatilia pia malengo mengine ya kiuchumi kupitia mauzo ya silaha. Kwa mantiki hiyo, Doha mbali na masuala ya kisasa inafanya juhudi za kuinua uwezo wake wa kijeshi kwa ajili ya kukabiliana na Saudi Arabia. Nukta inayofaa kuashiria hapa ni kwamba kuimarishwa mahusiano baina ya Russia na nchi za Kiarabu kama vile Qatar kwa ajili ya siasa za eneo la Mashariki ya Kati, kunamaanisha kwamba baadhi ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati ikiwemo Qatar yenyewe zimefikia natija hii kwamba, Washington sio mshirika wa kuaminika kwa ajili ya kuzidhaminia usalama nchi hizo. Ni kwa ajili hiyo ndipo Qatar ikaupa kipaumbele uhusiano wake na Russia.