UNRWA: Wapalestina Ghaza wanakabiliwa na hali mbaya kibinadamu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i42356-unrwa_wapalestina_ghaza_wanakabiliwa_na_hali_mbaya_kibinadamu
Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi wa Palestina Bw. Pierre Krahenbuhl ameonya kuhusu kuendelea kuwa mbaya hali ya kibinadamu ya Wapalestina katika eneo la Ukanda wa Gaza ambalo liko chini ya mzingiro wa Utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 29, 2018 02:06 UTC
  • UNRWA: Wapalestina Ghaza wanakabiliwa na hali mbaya kibinadamu

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi wa Palestina Bw. Pierre Krahenbuhl ameonya kuhusu kuendelea kuwa mbaya hali ya kibinadamu ya Wapalestina katika eneo la Ukanda wa Gaza ambalo liko chini ya mzingiro wa Utawala wa Kizayuni wa Israel.

Akizungumza na wanahabari katika mji wa Khan Younis kusini mwa Ghaza, Krahenbuhl amesema dunia inapaswa kusikiliza kilio cha Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza huku akitaka suala la mzingiro wa eneo hilo litafutiwe suluhisho la kisiasa.

Amesema shirika lake linafuatilia hali mabaya ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza kutokana na kuongezeka kwa kiasi kikubwa kwa kiwango cha ukosefu wa ajira na kushindwa kwa familia kukidhi mahitaji ya maisha ya kawaida.

Tokea mwaka 2007, utawala haramu wa Israel uliweka mzingiro wa anga, nchi kavu na baharini dhidi ya Ukanda wa Ghaza baada ya Wapalestina katika eneo hilo kuichagua kidemokrasia harakati ya Hamas kuongoza eneo hilo.

Makao makuu ya Unrwa katika Ukanda wa Ghaza

Mzingiro huo umelifanya eneo hilo lenye watu karibu milioni moja na nusu kutajwa kuwa gereza kubwa zaidi la wazi duniani. Misri inashirikiana na Israel katika kuwawekea Wapalestina mzingiro kwani njia ya nchi kavu inayounganisha Ghaza na nchi zingine duniani ni kupitia mipaka ya Misri.

Mbali na mzingiro huo, utawala haramu wa Israel pia umeanzisha vita mara tatu dhidi ya Ghaza tokea mwaka 2008 ambapo maelfu ya Wapalestina wakiwemo wanawake na watoto wameuawa mbali na miundo mbinu ya eneo hilo kama vile mahospitali, shule na nyuma za makazi kuharibiwa.