Hizbullah: Matukio ya Ghaza yamethibitisha kwamba matukufu ya Palestina bado yanaenziwa
Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon imetoa taarifa kufuatia maandamano makubwa ya Ijumaa ya jana mjini Ghaza Palestina na kusema kuwa, matukio hayo yamethibitisha kwamba matukufu ya Palestina bado yanaendelea kuenziwa na kwamba Wapalestina wako tayari kujitolea kila kitu chao katika njia ya ukombozi wa ardhi zao.
Katika taarifa yake hiyo iliyoitoa jana usiku Hizbullahi ya Lebanon imeonyesha masikitiko yake kufuatia kuuawa shahidi Wapalestina kadhaa na imetangaza mshikamano wake daima na raia madhlumu wa Palestina huku ikisisitiza kuwa, jihadi na muqawama dhidi ya wavamizi wa Kizayuni, ndiyo njia pekee ya kufikia ushindi wao kamili.
Aidha harakati hiyo ya Hizbullah imeyasifu maandamano ya jana ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza na kusema kwamba yalikuwa ya hamasa na kujitolea na imeongeza kuwa taifa la Palestina limeendelea kusimama imara kwa damu ya mashahidi, muqawama na kwa kupaza sauti yake juu. Aidha ripoti hiyo imesema, maandamano ya jana ya Siku ya Ardhi yaliyohimiza kurejea makwao Wapalestina na ambayo yalifanyika kwa ushiriki mkubwa wa Wapalestina, yameingiza katika mioyo ya maadui hali ya kukata tamaa na wasi wasi. Pia Hizbullah imetoa mkono wa pole kwa familia za mashahidi waliouliwa na askari katili wa utawala wa Israel na kuwatakia afya njema mamia ya Wapalestina waliojeruhiwa, kama ambavyo pia imewalaumu watu wanaojigamba kupigania haki dunia yakiwemo mataifa ya Kiarabu na ya Kiislamu kwa kutochukua hatua za maana kuhusu suala hilo.
Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah nchini Lebanon imewataka Wapalestina kuendeleza mapambano yao kwa ajili ya kuzikomboa ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na utawala bandia wa Israel na pia kuidhibiti upya Baitul-Muqaddas. Katika maandamano ya jana kwa akali Wapalestina 15 waliuawa shahidi na wengine 1100 kujeruhiwa. Tarehe 30 Machi ya kila mwaka inaitwa 'Siku ya Ardhi' ambapo hufanyika maandamano makubwa kwa ajili ya kutaka Wapalestina kurejea makwao.