Netanyahu awashukuru askari katili wa Israel waliowaua Wapalestina Ghaza
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amewapongeza na kuwashukuru wanajeshi wa utawala huo haramu waliowaua na kuwajweruhiwa mamia ya Wapalestina waliokuwa wakifanya maandamano ya amani hivi karibuni katika mpaka wa Ghaza, kushinikiza kurejea katika ardhi zao zilizoghusubiwa.
Katika ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Benjami Netanyahu amedai kuwa, kitendo alichokiita eti cha kishujaa kilichofanywa na wanajeshi wa Israel cha kulinda ardhi zao ni cha kupongezwa.
Hii ni licha ya jamii ya kimataifa kulaani vikali mauaji hayo ya kikatili yaliyofanywa na askari hao wa Israel.
Kwa akali Wapalestina 17 waliuawa shahidi juzi Ijumaa baada ya kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel waliokuwa wakikandamiza maandamano ya amani ya Siku ya Ardhi katika Ukanda wa Ghaza.
Aidha mamia ya wengine walijeruhiwa katika maandamano hayo ya amani ya kutaka haki ya kurejea katika ardhi zao zilizoporwa na utawala huo ghasibu.
Sambamba na kulaani vikali mauaji hayo, Rais Recep Tayyip Erdogan amehoji, "Je mmesikia kauli yoyote ya maana ya kupinga na kulaani mauaji ya Wapalestina wa Ghaza kutoka kwa wale wanaokosoa operesheni za Afrin?"
Tarehe 20 Januari mwaka huu, Uturuki ilivamia maeneo ya kaskazini mwa Syria kuendesha kila kinachodaiwa ni "Operesheni ya Tawi la Mzaituni" kwa madai ya kupambana na wanamgambo wa Kikurdi wanaoungwa mkono na Marekani.