Walowezi wa Kizayuni wauhujumu na kuuvunjia heshima Msikiti wa Al Aqsa
Mamia ya walowezi wa Kizayuni, wakiwa wanalindwa na askari wa utawala haramu wa Israel, wameuhujumu na kuuvunjia heshima Msikiti wa Al Aqsa kwa kupitia lango la al-Maghareba.
Taarifa zinasema hujuma hiyo ambayo ilitekelezwa jana Jumapili kwa munasaba wa siku ya Pasaka ilifanyika huku askari wa utawala haramu wa Israel wakiwazuia Wapalestina kuingia katika msikiti huo. Hujuma hiyo katika Msikiti wa Al Aqsa , ambao uko katika mji wa Al Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala wa Israel imefanyika baada ya wakuu wa utawala huo ghasibu kuweka vizingiti msikitini hapo katika kipindi cha Pasaka.
Wazayuni wamekuwa wakitekeleza njama za kuuhujumu mara kwa mara Msikiti wa Al Aqsa kwa lengo la kuwazuia Waislamu kuingia katika mstikiti huo ili hatimaye kubadilisha muundo wake na kuufanya kuwa wa Kiyahudi.
Kwa kuzingatia mipango ya ujenzi na ramani bandia walizonazo Wazayuni, inatabiriwa kuwa, iwapo mpango wa kuugawa Msikiti wa Al Aqsa utatekelezwa kikamilifu kutaibuliwa maeneo mengi bandia yatakayopewa majina ya Kiyahudi katika eneo la msikiti huo na natija ya hilo hatimaye itakuwa ni kutekelezwa njama ya kuubomoa kikamilifu msikiti huo ambao ni eneo la tatu kwa utukufu katika Uislamu. Waplestina wameutaka umma wa Kiislamu kuchukua hatua za haraka za kuuhami na kuulinda msikiti wa al-Aqsa na njama za utawala wa Kizayuni. Hata hivyo ombi hilo la Palestina si tu kuwa halijapokelewa na nchi za Kiarabu, bali sasa Saudi Arabia, ambayo inajidai kuwa eti mhudumu wa Haram Mbili za Kiislamu, inaongoza mkakati wa kuwa na uhusiano wa karibu na Wazayuni pamoja na utawala haramu wa Israel.