Wapalestina wamlaani Mrithi wa Ufalme Saudia kwa kutumikia Israel
Makundi ya kupigania ukombozi wa Wapalestina yamelaani vikali matamshi ya Mrithi wa Ufalme wa Saudia Mohammad bin Salman kufuatia hatua yake ya kutangaza kuwa anautambua utawala haramu wa Israel na kusema tamko hilo linakiuka wazi malengo matukufu ya Wapalestina.
Katika taarifa Talal Abu Dharifa, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Kidemokrasia kwa Ajili ya Ukombozi wa Palestina amelaani matamshi ya bin Salman aliyoyatoa katika mahojiano na Jarida la Atlantic la Marekani na kusema, matamshi hayo ni ishara ya wazi kuwa malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina yanakabiliwa na hatari kubwa. Nayo harakati ya Swabirin ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza, imesema matamshi ya bin Salman ni kukiri wazi mtazamo wa Saudia kuwa, ardhi za Palestina zinapaswa kukaliwa kwa mabavu. Aidha imesema matamshi hayo ni tangazao la wazi na bayana la kuanzisha uhusiano baina ya Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Harakati hiyo ya Palestina pia imelaani vikali hatua ya Bin Salman ya kuitaja Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, kuwa eti ni kundi la kigaidi sambamba na madai kuwa eti Hizbullah ni hatari kwa eneo.
Nayo Kamati Kuu ya Harakati ya Wananchi kwa Ajili ya Ukombozi wa Palestina imesema tamko la Bin Salman limelenga kuweka wazi uhusiano wa siri ambao umekuwepo kwa muda mrefu baina ya Israel na Saudia.
Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Ufalme wa Saudia, katika mahojiano na Jarida la Atlantic la Marekani amesema Saudia na utawala haramu wa Israel zina maslahi ya pamoja na iwapo zitakuwa na uhusiano wa wazi, basi utawala huo bandia utapata faida kubwa na pia nchi za Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi nazo zitafaidika eti kama ambavyo Misri na Jordan zimenufaika na uhusiano wao na utawala wa Tel Aviv.
Katika mahojiano hayo, Bin Salman hakuashiria hata kidogo mauaji ya umati yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina siku ya Ijumaa.