Marekani yaafiki kuiuzia Saudia silaha licha ya mauaji ya Wayemeni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i42712-marekani_yaafiki_kuiuzia_saudia_silaha_licha_ya_mauaji_ya_wayemeni
Washington imekubali kuiuzia Riyadh mifumo 180 ya mizinga yenye thamani ya dola bilioni 1.31 ikiwa ni katika mwendelezo wa Marekani wa kuiuzia Saudia silaha za mabilioni ya dola.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 06, 2018 03:14 UTC
  • Marekani yaafiki kuiuzia Saudia silaha licha ya mauaji ya Wayemeni

Washington imekubali kuiuzia Riyadh mifumo 180 ya mizinga yenye thamani ya dola bilioni 1.31 ikiwa ni katika mwendelezo wa Marekani wa kuiuzia Saudia silaha za mabilioni ya dola.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani jana ilitangaza kuwa imeidhinisha mauzo hayo ya silaha kwa Saudi Arabia. Kongresi ya Marekani ina muda wa siku 30 kupasisha mauzo hayo ya silaha  kwa Saudia.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani siku kadhaa zilizopita iliafiki pia Washington kuiuzia Saudia silaha zenye thamani ya dola bilioni moja ambazo ni pamoja na makombora 6,600 dhidi ya vifaru aina ya TOW.  Itakumbukwa kuwa akiwa ziarani mjini Riyadh mwaka jana wa 2017, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa, Saudi Arabia itanunua silaha zenye thamani ya dola bilioni 110 kutoka Marekani. Aidha katika mazungumzo yake hivi majuzi na Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia huko White House, Trump aliitaka Saudia izidishe ununuaji silaha kutoka Marekani. 

Bin Salman akiwa na mwenyeji wake Rais Donald Trump wa Marekani 

Ushirikiano wa kijeshi baina ya Marekani na Saudi Arabia unakabiliwa na upinzani mkubwa ndani ya Marekani kwenyewe. Sambamba na safari hiyo ya mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia nchini Marekani, kuliwasilishwa muswada katika Kongresi ya nchi hiyo ambao iwapo ungepasishwa, ungehitimisha uungaji mkono wa Washington kwa muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita huko Yemen.