Kaburi la umati lagunduliwa Palmyra, nchini Syria
Jeshi la Syria limegundua kaburi la umati ambalo lilikuwa limefukiwa makumi ya watu waliouawa na kundi la kigaidi na kitaifiri la Daesh katika mji uliokombolewa hivi karibuni wa Palmyra.
Shirika la Habari la Syria SANA, limenukuu duru za kijeshi zilizosema kuwa, miili 25 ikiwemo ya wanawake watano na watoto watatu imepatikana katika kaburi hilo.
Habari zinasema kuwa, jeshi la Syria liligundua kaburi hilo jana Ijumaa wakati lilipokuwa likifanya operesheni ya kutegua mabomu na mada za miripuko zilizotegwa ardhini na matakfiri wa Daesh.
Rais Bashar al-Assad wa Syria amelipongeza jeshi la nchi hiyo kwa kuukomboa mji wa kihistoria wa Palmyra kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh na kusisitiza kuwa, kukombolewa mji huo ni mafanikio makubwa sana kwa taifa la Syria na kwamba kunaonyesha namna jeshi la nchi hiyo likishirikiana na makundi ya wananchi linavyoendelea kupata mafanikio na kuzidi kukomboa miji mbali mbali ambayo ilikuwa chini ya udhibiti wa matakfiri wa Daesh.
Itakumbukwa kuwa, Juni mwaka jana 2015, wanachama wa kundi la kitakfiri la Daesh walibomoa makaburi mawili ya kale ya Mawalii wa Allah katika mji wa kihistoria wa Palmyra mkoani Homs nchini Syria.