Taarifa ya NAM ya kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i42750-taarifa_ya_nam_ya_kulaani_jinai_za_israel_dhidi_ya_wapalestina
Taarifa ya mwisho ya mkutano wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) uliofunga shughuli zake jana Ijumaa katika mji mkuu wa Azerbaijan Baku, imelaani sera zilizo kinyume cha sheria za utawala wa Kizayuni wa Israel, huku ikisisitiza juu ya udharura wa kuwepo jitihada za pamoja za kutamatisha ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 07, 2018 03:09 UTC
  • Taarifa ya NAM ya kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina

Taarifa ya mwisho ya mkutano wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) uliofunga shughuli zake jana Ijumaa katika mji mkuu wa Azerbaijan Baku, imelaani sera zilizo kinyume cha sheria za utawala wa Kizayuni wa Israel, huku ikisisitiza juu ya udharura wa kuwepo jitihada za pamoja za kutamatisha ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Palestina.

Sanjari na kulaani mauaji ya makumi ya Wapalestina wanaofanya maandamano tangu Ijumaa ya wiki jana katika mpaka wa Gaza, NAM imesema, "Tunalaani sera za ukaliaji wa mabavu wa Israel katika ardhi za Wapalestina, kughusubiwa ardhi za Wapalestina, kuendelezwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi hizo, kubomolewa nyumba za Wapalestina na kuharibiwa mali zao, dhulma dhidi ya jamii yote ya Wapalestina kukiwemo kufungwa jela na kuzuiliwa kinyume cha sheria, sambamba na mzingiro wa kibaguzi katika Ukanda wa Gaza."

Kadhalika taarifa hiyo ya NAM imelaani jitihada zozote za kuitambua Quds Tukufu kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel huku ikizionya nchi zinazotaka kuhamishia balozi zao kwenye mji huo kutoka Tel Aviv.

Zaidi ya Wapalestina 30 wameuawa hadi sasa katika maandamano ya "Haki ya Kurejea"

Akihutubu siku ya Alkhamisi katika mkutano huo, Mohammad Javad Zarif,  Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema utawala wa Kizayuni wa Israel ndilo tishio kubwa zaidi kwa usalama wa dunia. Sambamba na kulaani hatua ya vikosi vya usalama vya Israel ya kuwaua na kuwajeruhi mamia ya Wapalestina wa Ghaza, alisisitiza kuwa kuna udharura wa kuanzishwa uchunguzi mara moja juu ya ukatili huo.

Mkutano wa ngazi ya mawaziri wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) ulifunguliwa Alkhamisi, kwa kuwaleta pamoja wawakilishi 800 kutoka nchi wanachama 120, nchi 17 wanachama watazamaji, pamoja na asasi 10 za kimataifa, chini ya kaulimbiu "Kuunga mkono amani na usalama wa kimataifa, kwa ajili ya maendeleo-endelevu".