Israel: Tutaishambulia Hamas iwapo maandamano ya Gaza yataendelea
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i42800-israel_tutaishambulia_hamas_iwapo_maandamano_ya_gaza_yataendelea
Utawala wa Kizayuni wa Israel umetishia kuishambulia Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, iwapo Wapalestina wataendelea na maandamano yao katika mpaka wa Gaza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 08, 2018 03:19 UTC
  • Israel: Tutaishambulia Hamas iwapo maandamano ya Gaza yataendelea

Utawala wa Kizayuni wa Israel umetishia kuishambulia Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, iwapo Wapalestina wataendelea na maandamano yao katika mpaka wa Gaza.

Gazeti la Kizayuni la Haaretz limenukuu duru za kijeshi za Israel zikisema kuwa, vikosi katili vya utawala huo haramu vimejiweka tayari kuishambulia Hamas, ambayo inaendesha Ukanda wa Gaza.

Aidha walenga shabaha wa jeshi la Israel wameagizwa kumfyatulia risasi na kumuua Mpalestina yeyote atakayeonekana karibu na mpaka wa Gaza.

Wapalestina wasiopungua 30 wameshauawa shahidi hadi sasa na wengine zaidi ya 1,900 wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi na askari wa utawala haramu wa Israel tangu yalipoanza maandamano ya siku ya ardhi yaliyopewa jina la "Haki ya Kurejea" yaliyoanza huko Gaza Ijumaa ya Machi 30.

Vijana wa Kipalestina katika mpaka wa Gaza

Hii ni katika hali ambayo, Dakta Mahmoud al-Zahar, mjumbe wa ngazi za juu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas alisema hivi karibuni kwamba, Wapalestina wameazimia kufanya maandamano makubwa ya haki ya kurejea makwao Wapalestina na kwamba, vitisho vya Israel haviwezi kuwafanya waachane na uamuzi wao huo.

Tangu Januari mwaka 2006 na kufuatia ushindi wa harakati ya Hamas katika uchaguzi wa Bunge la Palestina, utawala wa Kizayuni wa Israel uliliwekea eneo la Ukanda wa Gaza mzingiro wa angani, baharini na nchi kavu kwa lengo la kuisambaratisha harakati hiyo ya muqawama.