Syria: Sheria za kimataifa hazina thamani yoyote kwa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i42936-syria_sheria_za_kimataifa_hazina_thamani_yoyote_kwa_marekani
Balozi na mwakilishi wa Syria katika Umoja wa Mataifa amekosoa matamshi ya vitisho yaliyotolewa na Marekani katika Baraza la Usalama la umoja huo na kueleza kuwa baraza hilo na misingi ya sheria za kimataifa havina thamani yoyote ile kwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 11, 2018 00:06 UTC
  • Syria: Sheria za kimataifa hazina thamani yoyote kwa Marekani

Balozi na mwakilishi wa Syria katika Umoja wa Mataifa amekosoa matamshi ya vitisho yaliyotolewa na Marekani katika Baraza la Usalama la umoja huo na kueleza kuwa baraza hilo na misingi ya sheria za kimataifa havina thamani yoyote ile kwa nchi hiyo.

Bashar Al-Jaafari ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Usalama na kufafanua kwamba Marekani inayapelekea silaha na zana za kivita makundi ya kigaidi nchini Syria ambayo yamewatendea wananchi wa nchi hiyo jinai kubwa zaidi za kinyama. Al-Jaafari aidha amelaani shambulio la Israel dhidi ya kituo cha anga cha T-4 mkoani Homs na kueleza kwamba hujuma hiyo ambayo ni ukiukaji wa wazi wa azimio nambari 350 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imesababisha idadi kadhaa ya raia wa Syria kuuawa shahidi na kujeruhiwa.

Mwakilishi wa Syria katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa: shambulio hilo la Israel ni jibu lisilo la moja kwa moja dhidi ya mafanikio liliyopata jeshi la taifa la Kiarabu la Syria la kuyafurusha makundi ya kigaidi yanayobeba silaha kandokando ya mji mkuu Damasacus na maeneo mengine ya nchi.

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Bashar Al-Jaafari amebainisha kwamba, uongo unaosemwa na baadhi ya wanachama wa Baraza la Usalama ni mithili ya silaha za mauaji ya umati, kwa sababu kwa uongo zinaosema, nchi hizo zinafanya njama ya kutoa pigo la kuidhuru Syria na kuandaa mazingira ya kuishambulia kijeshi.

Mwakilishi wa Syria katika Umoja wa Mataifa amesema serikali ya Damascus iko tayari kuandaa mazingira haraka iwezekanavyo ya kuifungulia njia kamati ya kutafuta ukweli ya Shirika la Upigaji Marufuku Silaha za Kemikali kwenda kufanya uchunguzi huko Duma kwenye eneo linalodaiwa kutumiwa silaha za kemikali na jeshi la nchi hiyo.../