HAMAS: Taarifa ya kikao cha "Dhahran" haikukidhi matakwa ya Wapalestina
Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema misingi thabiti ya taifa la Palestina ambayo ni misingi ya mataifa yote inayojumuisha watu, ardhi, itikadi na matakufu yao imepuuzwa katika taarifa iliyotolewa kwenye kikao cha viongozi wa nchi za Kiarabu kilichofanyika Dhahran, Saudi Arabia.
Kikao cha 29 cha viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kilifanyika Jumapili tarehe 15 Aprili katika mji wa Dhahran, mashariki mwa Saudia.
Mahmoud Az-Zahar amelieleza shirika la habari la Tasnim kuwa matakwa ya Wapalestina hayakuzingatiwa katika kikao cha viongozi wa nchi wanachama wa Arab League na kusisitiza kwamba kupuuzwa matakwa hayo yanayohusiana na haki ya wakimbizi kurejea kwenye ardhi ya asili ya Palestina, kuwatimua maghasibu wanaoikalia ardhi hiyo kwa mabavu na kukombolewa Quds tukufu kunadhihirisha njama chafu inayofanywa na Saudi Arabia ya kuifuta kadhia ya Palestina.
Dakta Az-Zahar amesema, amesikitishwa na kitendo cha Saudia na tawala nyingine za Kiarabu cha kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel na kuongeza kuwa msimamo huo unachukuliwa katika hali ambayo kila mtu anaelewa fika kwamba mfalme wa Saudia, Salman bin Abdulaziz ameafiki mpango wa Marekani unaojulikana kama "Mapatano ya Karne".
Katika kutekeleza mpango huo mpya wa Marekani ambao lengo lake ni kuifuta kadhia ya Palestina, tarehe 6 Desemba 2017, Rais Donald Trump wa Marekani aliitangaza Quds tukufu inayokaliwa kwa mabavu kuwa mji mkuu wa utawala bandia wa Israel na kueleza azma aliyonayo ya kuuhamishia kwenye mji huo ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv.
Kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas ameashiria pia jinsi utawala wa Kizayuni ulivyotetemeshwa na maandamano ya Wapalestina ya kupigania haki yao ya kurejea kwenye ardhi zao za asili yanayofanyika kwenye mpaka wa eneo lililowekewa mzingiro la Ukanda wa Gaza na kueleza kwamba, kuendelea maandamano hayo katika eneo lililoharibiwa kwa vita la Ukanda wa Gaza ni dhihirisho la kuendelea mapambano ya Wapalestina dhidi ya wavamizi na maghasibu wa Kizayuni na pia ni kielelezo cha utayarifu mkubwa zaidi walionao wa kujitoa mhanga katika njia ya machaguo manne yasiyoweza kubadilika ambayo ni kuendeleza muqawama na kupigania ardhi, imani na matukufu yao.../