Umoja wa Ulaya waitaka Israel ikomeshe unyama wake dhidi ya Wapalestina
Umoja wa Ulaya umeutaka utawala ghasibu wa Israel ukomeshe vitendo vyake vya utumiaji mabavu dhidi ya Wapalestina.
Taarifa ya Umoja wa Ulaya sambamba na kulaani ukandamizaji wa hivi karibuni wa jeshi la Israel umeutaka utawala huo wa Kizayuni kukomesha vitendo vyake hivyo dhidi ya Wapalestina.
Taarifa hiyo ya Umoja wa Ulaya imetolewa baada ya walimwengu kushuhudia katika majuma ya hivi karibuni ukandamizaji dhidi ya Wapalestina ukiongezeka.
Juzi Ijumaa Wapalestina wanne waliokuwa wakishiriki katika maandamano ya amani katika Ukanda wa Gaza waliuawa shahidi kwa risasi za utawala ghasibu wa Israel, huku wengine zaidi ya 40 wakijeruhiwa, na hivyo kupelekea idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi kufikia sasa kupindukia 35, katika kipindi cha wiki tatu.
Maandamano ya amani ya 'Haki ya Kurejea' yaliyoitishwa na Wapalestina kwa ajili ya kupigania haki ya kurejea wakimbizi wa taifa hilo katika ardhi zao walizoporwa na Wazayuni mwaka 1948 yalianza Machi 30, na yanatazamiwa kuendelea hadi Mei 15.
Nchi mbalimbali duniani zimeendelea kulaani jinai hizo za Israel na kutaka kuundwa kamisheni huru ya kuchunguza jinai za kutisha zinazofanywa na wanajeshi katili wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.