Mwanahistoria mashuhuri wa Kiyahudi: Marekani imewafanyia hadaa watu wa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i43998-mwanahistoria_mashuhuri_wa_kiyahudi_marekani_imewafanyia_hadaa_watu_wa_palestina
Mwanahistoria mtajika wa Kiyahudi Ilan Pappé ameashiria jinsi baadhi ya Wapalestina walivyodhani kwamba Marekani ikiwa kama mpatanishi itasaidia mpango wa kuundwa nchi ya Palestina na kubainisha kuwa serikali za Marekani ikiwemo ya Barack Obama zimewafanyia hadaa watu wa Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 03, 2018 10:39 UTC
  • Mwanahistoria mashuhuri wa Kiyahudi: Marekani imewafanyia hadaa watu wa Palestina

Mwanahistoria mtajika wa Kiyahudi Ilan Pappé ameashiria jinsi baadhi ya Wapalestina walivyodhani kwamba Marekani ikiwa kama mpatanishi itasaidia mpango wa kuundwa nchi ya Palestina na kubainisha kuwa serikali za Marekani ikiwemo ya Barack Obama zimewafanyia hadaa watu wa Palestina.

Ilan Pappé ameyasema hayo mjini Doha, Qatar na kufafanua kuwa licha ya baadhi ya Wapalestina wa Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan kuwa na dhana kwamba njia ya uundaji nchi mbili itahitimisha ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na Wazayuni lakini misimamo iliyotangazwa hivi karibuni na Marekani imeonyesha kuwa serikali ya Washington haiwezi kutoa mchango chanya na athirifu katika machakato wa mapatano.

Mwanahistoria huyo wa Kiyahudi aidha amesema mchakato wa mapatano unafuatilia mipango isiyojali maslahi na manufaa ya Wapalestina na kubainisha kuwa uamuzi wa serikali ya Marekani wa kutaka kuuhamishia mji wa Quds ubalozi wake ulioko Tel Aviv ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Mtaalamu na mchambuzi huyo wa Kiyahudi ameongeza kuwa Marekani imesababisha kupanuka Kampeni ya Uzayuni katika ardhi ya Palestina na kuulinda mpango huo kupitia ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina

Ilan Pappé vilevile amebainisha kwamba hatua ya rais wa Marekani, Donald Trump ya kuitangaza Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni imewathibitishia Wapalestina kuwa Washington haina nia ya kusaidia mpango wa kuundwa nchi huru ya Palestina.

Ikumbukwe kuwa tangu Trump alipotangaza uamuzi huo tarehe 6 Desemba mwaka jana, hadi sasa Wapalestina 104 wameuliwa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.../