Jeshi la Syria lanasa silaha za Israel ilizowapa magaidi wakufurishaji
Jeshi la Syria limepata idadi kubwa ya silaha, zikiwemo za kemikali, ambazo utawala haramu wa Israeli, ulikuwa umewapa magaidi wakufurishaji nchini humo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Sputnik, katika oparesheni za kuwatimua magaidi kutoka mkoa wa Homs yapata kilomita 162 kutoka, Damascus, Jeshi la Syria limegundua shehena kubwa ya silaha, zikiwemo za kemikali, dawa za kulevya, na vifaa vya kielektroniki. Taarifa zinasema shehena hiyo kubwa ya silaha ilikuwa iwafikie magaidi wakufurisahji wanaopingia serikali wakiwemo magaidi wa ISIS au Daesh.
Hii si mara ya kwanza kwa Syria kunasa silaha za Israel zikiwa mikononi mwa magaidi wa Kiwahhabi ambao wanapata himaya ya kigeni katika njama yao ya kutaka kuipindua serikali halali ya Rais Bashar al Assad.
Mwezi Oktoba mwaka jana, maghala kadhaa makubwa ya silaha za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel yaligunduliwa katika maficho ya genge la kigaidi la ISIS katika mji uliokombolewa wa al Mayadin mkoani Dayr al-Zawr, mashariki mwa Syria.
Tangu ulipoanzishwa mgogoro wa Syria mwaka 2011, daima utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani pamoja na vibaraka wao katika eneo, hasa Saudi Arabia, wamekuwa wakiwasaidia kwa kila namna magaidi wanaofanya jinai za kutisha nchini Syria.