Tofauti na mapigano katika safu ya magaidi nchini Syria
Sambamba na kusonga mbele jeshi la Syria kwa kushirikiana na muqawama, watetezi wa haki za binaadamu nchini humo wameelezea kuanza mapigano kati ya makundi mawili ya wabeba silaha na yanayoungwa mkono na Marekani kaskazini mwa mkoa wa Idlib, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Watetezi wa haki za binaadamu nchini Syria wenye mafungamano na wapinzani dhidi ya serikali ya Damascus wametangaza kuwa, kufuatia pendekezo la wapiganaji wa chama cha Demokrasia cha Kikurdi wa Syria la kuwataka wapiganaji wa Nukhbah wa Ahmad al-Jaraba, mkuu wa harakati ya upinzani ya al-Ghad, kusini mashariki mwa Deir ez-Zor, mashariki mwa Syria kukabidhi silaha zao, wanachama wa makundi mawili hayo wameshambuliana vikali mkoani Idlib. Wapiganaji wa Nukhbah, ni magaidi ambao walipewa mafunzo ya kijeshi na askari wa Marekani na Uingereza nchini Jordan na kabla ya hapo walikataa kuunganishwa na wapiganaji wa Kikurdi wa nchini Syria.
Kufuatia kushindwa mtawalia magaidi wa Syria katika maeneo tofauti na kusonga mbele jeshi la serikali na wanamapambano wa muqawama wa harakati ya Hizbullah, tofauti kati ya viongozi wa makundi hayo zimezidi kuongezeka. Katika matukio mengine, Muhammad Alloush, kiongozi wa ofisi ya kisiasa ya kundi la kigaidi linaloitwa, Jaishul-Islam pia ametangaza kujiuzulu cheo chake hicho ndani ya kundi hilo la ukufurishaji. Kujiuzulu Alloush katika nafasi hiyo kumejiri katika hali ambayo mwezi Aprili uliopita wanachama wa kundi la Jaishul-Islam walijisalimisha eneo la Ghouta Mashariki, sambamba na kulazimika kukubali masharti ya jeshi la Syria kwa ajili ya kuondoka katika mji wa Douma na vitongoji vya mji wa Al-Qalamoun Mashariki, hatua ambayo ilienda sambamba na kukabidhi kwao silaha nzito na kisha kuelekea mji wa Idlib na Jarabulus, kaskazini mashariki mwa mji wa Aleppo, kaskazini mwa Syria.
Aidha kujiuzulu na kujiengua kwa kila mara viongozi wa magenge ya kigaidi nchini Syria ambako kumekuwa kukifanyika kwa visingizio tofauti, kunabainisha hali ya mgogoro na tofauti kubwa zilizopo katika safu ya makundi hayo hasa baada ya kushindwa katika ulingo wa vita. Kusambaratishwa kundi la Daesh nchini Syria baada ya kukombolewa mji wa Al-Bukamal, ambao ulikuwa ngome ya mwisho ya genge hilo nchini Syria na ambako kulienda sambamba na kuanza kushindwa kikamilifu makundi mengine ya kigaidi na ya ukufurishaji ndani ya taifa hilo la Kiarabu, kumeakisiwa sana kisiasa na duru mbalimbali.
Suala hilo pamoja na mambo mengine limetafsiriwa na weledi wa mambo kuwa ni dhihirisho la uwepo wa tetemeko kubwa miongoni mwa makundi hayo lililosababishwa na kushindwa kwao kijeshi nchini humo. Katika miezi ya hivi karibuni, jeshi la Syria kwa kushirikiana na wanamuqawama limefanikiwa kutoa pigo zito kwa magaidi. Aidha kushindwa mtawalia makundi hayo katika kufikia malengo yao ya kisiasa na kijeshi nchini Syria, ndiko kumepelekea kuongezeka mapigano ndani ya safu ya magenge hayo sambamba na kuibuka mpasuko wa kisiasa baina yao. Na bila shaka mabadiliko hayo yataharakisha kuangamia kikamilifu makundi hayo katika eneo la Mashariki ya Kati. Inafaa kuashiria kuwa, hadi sasa bado kuna makumi ya makundi ya kigaidi nchini Syria yanayotumia majina tofauti na ambayo yanaungwa mkono na madola ya kigeni maarufu kwa kupanga njama chafu dhidi ya taifa hilo.
Makundi hayo na kwa tamaa tofauti yanajishughulisha na vita dhidi ya jeshi na raia wa Syria ambapo hata hivyo kutokana na kufeli njama za mabwana wao, yamejikuta yakishambuliana na kusababisha mauaji makubwa kati yao. Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa Syria al-Aana, kuendelea ongezeko la tofauti baina ya makundi ya kigaidi na viongozi wa magenge hayo katika eneo, kumeongeza pia mwenendo wa kusambaratika makundi hayo....Alaakullihal, kuendelea tofauti kati ya wapinzani wa serikali ya Syria hakuishii tu katika uga wa kijeshi na operesheni, bali mwenendo huo umeendelea kushika kasi pia katika uga wa kisiasa. Kwa kuzingatia hali hiyo, matukio ya Syria yanabainisha kuanza safu mpya kati ya magenge ya kigaidi na kushtadi tofauti kati yao siku hadi siku.