Ushindi wa Muqawama katika uchaguzi wa Lebanon wawatia kiwewe Wazayuni
Vyombo vya habari utawala wa Kizayuni wa Israel vimetangaza kuwa ushindi wa mrengo unaoongozwa na Hizbullah katika uchaguzi wa bunge la Lebanon unatia wasiwasi mkubwa.
Tovuti ya masuala ya usalama ya DEBKAfile yenye mfungamano na vyombo vya intelijinsia vya utawala wa Kizayuni wa Israel imeeleza kusikitishwa na matokeo ya uchaguzi wa bunge nchini Lebanon na kuandika kuwa: suala hili linaibua kambi ya pili kwa ajili ya Iran dhidi ya Israel baada ya ile ya Syria; na sasa inangojea kuilenga Israel kutokea kambi mbili za Syria na Lebanon.
Gazeti la Kizayuni la Maariv nalo limeandika kuwa Iran imepata karata nyingine ya turufu kwa ajili ya kukabiliana na Israel.
Gazeti la Israel Hayom limebainisha kuwa ushindi wa Hizbullah katika uchaguzi wa bunge la Lebanon umeiimarisha harakati hiyo na kuwatia wasiwasi viongozi wa Israel.
Nalo gazeti la Jerusalem Post limeuzungumzia ushindi wa Hizbullah katika uchaguzi kwa kuandika kuwa matokeo ya uchaguzi huo wa bunge yamezidi kuimarisha nafasi ya harakati hiyo ya muqawama katika vyombo vya upitishaji maamuzi na utekelezaji nchini Lebanon. Gazeti hilo la Kizayuni limeongeza kuwa: uchaguzi huo ni ishara ya kushindwa kifedheha muungano unaoungwa mkono na Magharibi mbele ya muungano unaoungwa mkono na Iran; na baada ya uchaguzi huo itakuwa zamu ya uchaguzi wa Mei 12 wa bunge nchini Iraq ambako huko pia kuna uwezekano wa kupatikana waziri mkuu anayeiunga mkono Iran.
Uchaguzi wa bunge la Lebanon ulifanyika siku ya Jumapili ya tarehe 6 Mei katika majimbo 15 ya uchaguzi. Mrengo wa mhimili wa Muqawama uliibuka mshindi kwa kujizolea viti 67 kati ya viti vyote 128 vya bunge la nchi hiyo.../