Walowezi wa Kizayuni wauhujumu Msikiti wa al Aqsa mjini Quds
Walowezi zaidi ya 300 wa Kizayuni wameuhujumu Msikiti wa al Aqsa ulioko katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Walowezi hao wa Kizayuni wamefanya hujuma hiyo na kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa, Kibla cha Kwanza cha Waislamu, huku wakiwa wanapewa ulinzi kamili na wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel.
Kwa mujibu wa Fira al-Debs, mkuu wa kitengo cha habari cha Wakfu wa Kiislamu wa Quds Tukufu, walowezi hao wa Kizayuni mapema Jumapili waliuhujumu Msikiti wa al Aqsa kupitia mlango wa Bab al-Magharibah huku wakiwa wamepewa ulinzi wa vikosi maalumu vya jeshi la Israel.
Debs amesema walowezi zaidi wa Kizayuni wanatazamiwa kuuhujumu msikiti huo leo Jumatatu kama sehemu ya sherehe ya Kiyahudu inayojulikana kwa jina la Shavout.
Ardhi za Palestina zimeshuhudia hali ya taharuki kubwa tokea rais wa Marekani Donald Trump atangaze Disemba mwaka jana kuwa ameitambua Quds kuwa eti ni mji mkuu wa utawala bandia wa Israel. Aidha Trump alitangaza kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Quds, uamuzi ambao umetekelezwa siku chache zilizopita na kuibua hasira za Wapalestina na Waislamu kote duniani mbali na kulaaniwa vikali na jamii ya kimataifa.