Saad al Hariri akabidhiwa jukumu la kuunda serikali mpya ya Lebanon
Saad al Hariri, Waziri Mkuu wa sasa wa Lebanon, ameteuliwa kuunda serikali mpya baada ya kujipatia kura nyingi za wabunge wa bunge la nchi hiyo.
Kanali ya televisheni ya Al Mayadeen imeripoti kuwa baada ya kuungwa mkono kwa kura 111 kati ya 128 za wabunge wote wa Bunge la Lebanon, Hariri amekabidhiwa jukumu la kuunda baraza jipya la mawaziri.
Mashauriano ya wabunge kwa ajili ya kumteua mtu atakayekabidhiwa jukumu la kuunda serikali mpya ya Lebanon, yalifanyika leo katika Ikulu ya rais ya Baabda katika kikao kilichohudhuriwa na rais wa nchi hiyo Michel Aoun.
Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon Najib Miqati amesisitiza kuwa katika mazingira yaliyopo nchini hivi sasa kuna haja ya kumteua tena Saad al Hariri kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo.
Hapo jana Bunge la Lebanon lilimchagua Nabih Berri kuwa Spika wa bunge hilo. Berri alifanikiwa kupata kura 98 kati ya kura zote 128 na hivyo kumuwezesha kuendelea kushikilia kiti cha uspika kwa muhula wa sita tokea mwaka 1992.
Berri hakuwa na mpinzani katika kuwania kiti cha uspika wa bunge ambacho kwa mujibu wa mpango wa kugawana madaraka Lebanon kinapaswa kushikiliwa na Mwislamu wa madhehebu ya Shia; nayo nafasi ya waziri mkuu ni lazima ishikiliwe na Mwislamu wa madhehebu ya Sunni na rais wa nchi naye anatakiwa atoke miongoni mwa Wakristo wa Maroni.../