Umoja wa kitaifa, suluhisho la changamoto za Lebanon
Baada ya bunge la Lebanon kumchagua kwa sauti moja, Sad Hariri, Waziri Mkuu wa hivi sasa, kubuni baraza la mawaziri, inatazamiwa kuwa baraza hilo pia litabuniwa kwa msingi wa kuimarisha uwiano na umoja wa kitaifa.
Sad Hariri amepewa jukumu la kubuni baraza jipya la mawaziri katika hali aambayo katika uchaguzi wa bunge wa hivi karibuni mrengo wake wa kisiasa yaani Mrengo wa 14 Machi, ambao ni wa makundi ya kisiasa yanayoungwa mkono na nchi za Magharibi, ulipata pigo kubwa katika uchaguzi huo kwa kupoteza viti vya bunge, ambapo wingi wa viti hivyo uliuendelea mrengo wa mapambano wa Machi 8 ambao unaundwa na makundi yanayopinga ubeberu wa nchi za Magharibi katika nchi hiyo ya Kiarabu. Ni kwa kuzingatia hali tata ya hivi sasa ya Lebanon na ukweli kuwa ni lazima waziri mkuu atoke katika jamii ya Wasuni na vilevile juhudi kubwa ambazo zimekuwa zikifanywa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah kwa ajili ya kurejesha utulivu wa kudumu nchini humo, ndipo Hariri akapewa fursa nyingine ya kubuni baraza la mawaziri.
Kuhusiana na suala hilo, Najib Miqati, Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon anathibitisha kwamba Hariri amepewa nafasi hiyo ya kubuni baraza jipya la mawaziri la Lebanon kutokana na hali maalumu inayotawala hivi sasa nchini humo. Hii ni katika hali ambayo Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon naye pia amepewa fursa nyingine ya kuhudumia nafasi hiyo ikiwa ni katika mkondo huohuo wa kuleta hali ya maelewano na umoja nchini. Hali ya utulivu ambayo inatawala kwa sasa nchini Lebanon kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na mrengo wa ushindi katika uchaguzi wa hivi karibuni, yaani Harakati ya Hizbullah, imepelekea maamuzi muhimu ya kisiasa kuchukuliwa kwa msingi wa mashauriano yanayofanyika kati ya makundi yote ya kisasa.
Suala hilo bila shaka litawapelekea Walebanoni wote kutumia uwezo wao wa kisiasa katika mkondo wa kuimarisha maendeleo ya nchi hiyo, mwenendo ambao bila shaka utawaweka Walebanoni katika njia ya ushirikiano wa kisiasa katika kukabiliana na changamoto muhimu zinazoikabili nchi hiyo na hasa za kiuchumi na vilevile kukabiliana na vitisho vinavyohatarisha usalama wa nchi hiyo hasa kutoka kwa utawala ghasibu wa Israel na makundi ya kitakfiri na kigaidi. Kuandaliwa kwa mafanikio uchaguzi wa hivi karibuni wa bunge la Lebanon na kuanza kazi kwa baraza jipya la mawaziri kumeimarisha mkondo wa demokrasia nchini humo, jambo ambalo bila shaka litakuwa na matokeo chanya katika kuimarisha usalama wa taifa hilo. Matukio ya hivi karibuni katika eneo yanatoa udharura wa kubuniwa haraka baraza la mawaziri la Lebanon kwa ajili ya kuimarisha umoja na mshikamano kati ya makundi tofauti ya nchi hiyo.
Kufanikiwa kwa jambo hilo bila shaka kunategemea uamuzi atakaouchukua Hariri mwenyewe katika kubuni Baraza lake la mawaziri. Ni wazi kuwa anatakiwa kubuni baraza lenye mawaziri walio na uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto muhimu za nchi hiyo na hasa za kiuchumi na kiusalama, na pia kuzingatia nafasi ya mrengo ulioshinda uchaguzi huo, katika kuwachagua mawaziri wake. Kwa kutilia maanani uamuzi wa wananchi wa Lebanon wa kuupa kura zao nyingi mrengo wa mapambano ya Kiislamu, Hariri anapasa kuwazingatia ipaswavyo wanachama wa mrengo huo na kuwapa nafasi nyingi za mawaziri, katika uteuzi wa baraza lake jipya la mawaziri.