Kifaru cha Israel chaua shahidi Wapalestina 3 Gaza
Kwa akali Wapalestina watatu wameuawa shahidi kufuatia shambulizi la kifaru cha utawala wa Kizayuni wa Israel mashariki mwa mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Wizara ya Afya ya Palestina imethibitisha kutokea hujuma hiyo ya kikatili leo Jumapili na kuwataja mashahidi wawili kati ya watatu waliouawa kama Hussein al-Amour, aliyekuwa na umri wa miaka 25, na Abdul Haleem al-Naqa, 28.
Taarifa ya wizara hiyo imefafanua kuwa, jeshi la utawala haramu wa Israel limelenga kituo cha upekuzi cha harakati ya muqawama ya Jihad Islami, kwa madai kuwa harakati hiyo imerusha kifaa kilicholipuka katika uzio wa Ukanda wa Gaza.
Hii ni katika hali ambayo, kijana mmoja wa Palestina aliuawa shahidi huku watu wengine 109 wakijeruhiwa katika maandamano ya 'Haki ya Kurejea' yaliyofanyika Ijumaa iliyopita katika Ukanda wa Gaza.
Maandamano ya amani ya 'Haki ya Kurejea' yalianza tarehe 30 Machi mwaka huu kwa mnasaba wa 'Siku ya Ardhi' na kwa ajili ya kupigania haki ya wakimbizi wa Kipalestina kurejea katika ardhi zao za jadi.
Maandamano hayo yamekuwa yakikabiliwa kwa mkono wa chuma na wanajeshi katili wa Israel, ambapo kufikia sasa Wapalestina 114 wameshauawa shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi hao dhalimu na karibu 13,000 wengine kujeruhiwa.