Israel kupitisha muswada wa kuficha jinai za askari wake
Utawala haramu wa Israel inajadili muswada wenye lengo la kuwalinda askari wake, kwa kuzuia picha na video zinazowaonyesha askari hao katili wakitenda jinai dhidi ya Wapalestina.
Gazeti la utawala huo la Haaretz limeandika kwamba kwa mujibu wa muswada huo, itakuwa ni marufuku kueneza kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari picha na video zinazoonyesha mashambulizi na hujuma za askari hao. Kadhalika kwa mujibu wa ripoti hiyo, iwapo mtu atakiuka sheria hiyo basi atakumbwa na kifungo cha miaka mitano jela. Utawala bandia wa Israel ambao umekuwa ukiyakalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina tangu mwaka 1948 Miladia, umekuwa ukitekeleza kila aina ya jinai na mauaji ya kutisha dhidi ya raia wanaodhulumiwa wa Palestina.
Aidha hatua ya Wazayuni ya kuenedeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi ndani ya maeneo na ardhi za Wapalestina, unakusudia kubadili muundo wa kijamii na kijografia wa maeneo hayo kwa maslahi ya utawala huo khabithi ili uweze kuimarisha uvamizi wake.