Magaidi wa Syria waendelea kuuana wakigombea maslahi
Mapigano yameendelea kati ya makundi ya kigaidi na ukufurishaji katika mkoa wa Idlib, Syria ambapo sasa wanatumia magari yaliyotegwa mabomu kushambuliana.
Jumamosi usiku gari lililotegwa mabomu liliripuka karibu na makao makuu ya chama kinachojiita 'Turkistan Islami' ambacho ni moja ya makundi ya kigaidi eneo la Jisr al-Shughur mkoani Idlib ambapo makumi ya wanachama wa kundi hilo waliuawa na kujeruhiwa. Kadhalika gari lingine lililotegwa mabomu liliripuka karibu na ngome ya magaidi wakufurishaji wa genge la Tahriru sh-Sham ambalo zamani lilikuwa likiitwa (Jab'hatu Nusra) katika mkoa huo na kusababisha maafa makubwa katika safu ya wanachama wa kundi hilo sambamba na kusababisha hasara kubwa ya mali.
Duru za habari zinaarifu kwamba makumi ya magaidi hao wameuawa na kujeruhiwa wakiwemo pia watoto wadogo. Mkoa wa Idlib nchini Syria umekuwa ukishuhudia mapigano katika miezi ya hivi karibuni kati ya wanachama wa magenge ya kigaidi ambayo yote yanapata uungaji mkono kutoka Marekani, Israel, Saudia na nchi nyingine za Kiarabu. Kwa mujibu wa habari za ndani ya makundi hayo, zaidi ya wanachama 4000 wamekwishauawa katika mapigano hayo ya pande mbili. Tofauti na mapigano katika safu ya magaidi nchini Syria yameshtadi baada ya jeshi la nchi hiyo kwa kushirikiana na muqawama kupata mafanikio makubwa katika uwanja wa vita dhidi ya magaidi.